Fuvu la Chifu Mkwawa

Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga maarufu Mtwa Mkwawa, alikuwa mtemi na kiongozi mkuu wa kabila la Wahehe wakati wa uvamizi wa ukoloni wa Ujerumani mwishoni mwa karne ya 19.

Alizaliwa 1855 na akaitwa Ndesalasi, maana yake ‘Mtundu au Mdadisi’
Katika utu uzima aliitwa Mtwa Mkwava Mkwavinyika Mahinya Yilimwiganga Mkali Kuvago Kuvadala Tage Matenengo Manwiwage Seguniwagula Gumganga, ikiwa na maana ya ‘Mtawala, mtekaji wa nyika, mkali kwa wanaume mpole kwa wanawake asiyetabirika, alieshindikanika, mbabe mwenye nguvu udongo pekee ndio utakomuweza’.

Alipewa jina hilo mnamo 1887, baada ya vita na kabila la Wangoni kutoka Songea, Wajerumani walishindwa kutamka ‘Mkwava’ na kumuita Mkwawa.Inaaminika kwamba chifu Mkwawa alijitoa uhai mwenyewe mnamo 1898, wakati alipokuwa akijificha katika pango la Mlambalasi lililozungukwa na wanajeshi wa Ujerumani hivyo hakutaka kukamatwa na Wajerumani hao akiwa hai.

Baada ya kujiua mwenyewe kwa Bunduki wajerumani walichukua kichwa chake na kukipeleka kwao japo awali Ujerumani ilikana kuwa ina fuvu la Chifu Mkwawa mpaka pale ilipogunduliwa kuwa fuvu hilo lipo katika mji wa Bremen Ujerumani.

Katika miaka ya 1950, gavana wa Uingereza wa iliyokuwa Tanganyika, Edward Twining, alikuwa mwepesi kuchukua hatua na kulirudisha fuvu hilo nchini Tanzania 19, Julai 1954 na kumkabidhi Chifu Adam Sapi ambaye alikuwa chifu wa wahehe kwa kipindi hicho na ndiye spika wa kwanza wa Bunge la Tanganyika.

Fuvu la Chifu Mkwawa limewekwa ndani ya sanduku la kigae katika jumba la makumbusho lililopo Kalenga Iringa.