KAKAKUONA, MNYAMA ANAYESIFIKA KWA UWEZO WAKE WA KUTABIRI

Pangolin ndio jina lake kwa lugha ya kigeni likiwa na asili ya Malaysia likimaanisha kitu kinachojiviringisha. 

Mnyama huyu wa ajabu ana uwezo wa kujiviringisha kama mpira hasa anapokuwa hatarini, mgongo wake umefunikwa na magamba makubwa na magumu ambayo pindi anapojiviringisha hutengeneza ngao inayomfunika na kumkinga dhidi ya makali ya makucha na meno ya wanyama wakali. 

Majina hutolewa kulingana na mazingira au tabia husika vivyo hivyo kwa mnyama huyu pia, kwa Kiswahili anaitwa Kakakuona. Jina hili ni kutokana na imani kuwa wanyama hawa wana uwezo wa kuona mambo yajayo. 

IMANI

Historia inatuambia zamani, huko nyanda za juu Kusini katika jamii ya Wasangu iliaminika kuwa Kakakuona ni viumbe walioanguka duniani kutoka angani na ni wajumbe waliotumwa na roho za mababu. Zaidi ya hayo, iliaminika kuwa kila Kakakuona akifika duniani  hushikamana na mtu binafsi na kumfuata hadi nyumbani. 

Lakini kama vile haitoshi jamii ilimchukulia Mtu ‘aliyechaguliwa’ na Kakakuona kama mtu aliyezaa mapacha.

Ikumbukwe enzi hizo mtu kuzaa mapacha halikuwa jambo zuri wala la kutamanika kama ilivyo sasa ambapo wanawake wengi hutamani na wengine hadi humuomba Mungu awape mapacha. 

Zamani wazazi wa mapacha walifanyiwa msururu wa ibada na matambiko ili kujiondolea balaa hilo kwani mapacha waliaminika kuwa na ishara mbaya kwenye jamii. Vivyo hivyo kwa vile mtu aliyechaguliwa na Kakakuona alichukuliwa kama mzazi wa mapacha, yeye na Kakakuona walilazimika kubaki nyumbani na kushiriki katika matambiko.

Simulizi za kihistoria zinaeleza kuwa baada ya nyimbo na ngoma za matambiko kunoga, Kakakuona pia hujiunga katika kucheza. Baadhi ya Kakakuona wanaripotiwa kumwaga machozi kwa wingi wakati wakicheza huku wengine wakiwa na macho makavu.

Kiafrika na kibantu kila kitu kinatafsiri yake, kumwaga machozi  ilitafsiriwa kama ishara ya mvua nzuri katika mwaka ujao huku macho kavu yaliaminisha wazee kuwa Kakakuona ameona ukame.

Hata sasa licha ya elimu na utandawazi imani hizi bado zinatenda kazi, pindi Kakakuona anapoonekana kwenye jamii, watu humzunguka na kumuekea vitu mbalimbali wakiamini chochote kitakachofatwa na Kakakuona ndicho kitakachotokea, akifata chakula basi utakuwa mwaka wa chakula na heri, akifata silaha basi utakuwa mwaka wa machafuko na vurugu.

Hizi zote ni imani, unachoamini ndicho kinachokuwa lakini kisayansi na etholojia Kakakuona ni mnyama wa kawaida kutoka familia ya Wahanga pekee wenye magamba ijulikanayo kama Manidea, huku tafiti  zikionesha  kuwa asilimia 20 ya uzito wake unatokana na magamba yake.

CHAKULA
Chakula kikuu cha Kakakuona ni wadudu hususani jamii ya mchwa na siafu ambao mara nyingi huishi kwenye vichuguu. Hivyo Kakakuona hulazimika kuchimba kwenye vichuguu kwa kutumia makucha yake na kupenyeza ulimi wake ili kufikia wadudu hao.

Kwa vile wadudu nao hujitajidi kukimbilia ndani zaid ya ya vichuguu, Kakakuona analazimika kunyoosha ulimi wake unaonata ili kuwafikia na kuwanasa. Kwa sababu hiyo Kakakuona ana ulimi  mrefu ambao akiunyoosha unafika sentimita 40 na hata zaidi. 

Hana meno hivyo wadudu wakinasa kwenye ulimi wake humezwa na kuendelea kumeng’enywa kikemikali zaidi.

KAKAKUONA HUFANYA SHUGHULI ZAKE WAKATI WA USIKU
Ni nadra sana kumuona Kakakuona, pengine ndio maana akahusishwa na imani za mababu, lakini kutokuonekana kwao kunachagizwa na utofauti wa ratiba kati ya Kakakuona na binadamu. 

Kiasili Mnyama huyu hufanya harakati zake usiku wakati ambao binadamu wamepumzika nyumbani mwao na mchana wakati binadamu anafanya shughuli zake wao hujipatia usingizi kwenye mashimo. 

MALEZI 
Kakakuona hapendi makundi mara nyingi huonekana akiwa peke yake na muda pekee ambao Kakakuona huonekana wakiwa wawili ni wakati wa kuzaliana au wakati wa malezi, anabeba mimba kwa muda wa miezi 5 na kuzaa mtoto mmoja tu kwa mwaka. 

Mtoto wa Kakakuona huzaliwa akiwa na Ngozi laini na huendelea kulelewa na mama yake mpaka atakapokomaa kujitegemea.

Wakati wanyama wengine wakibeba watoto mgongoni kakakuona anabeba mtoto wake kwenye mkia na mtoto hujishika vizuri bila kudondoka .

ULINZI
Ni vyema kuwa na mpango mbadala! Kakakuona akiona adui hujilinda kwa kujiviringisha, lakini akiona hali inakuwa mbaya zaidi, hutema sumu kali mithili ya tindikali inayoweza kumdhuru adui. Mapambano yakiwa makali zaidi Kakakuona hunyoosha mkia wake na kuuzungisha kwa lengo la kumkata adui aliyekaribu yake. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Hifadhi za Asili (IUCN) limemweka Kakakuona kwenye orodha ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka duniani kutokana na biashara ya wanyamapori iliyopelekea maelfu ya Kakakuona kukamatwa na kuuawa.

Viume hawa wenye magamba wanabeba jukumu kubwa katika mazingira . Kupitia tabia yao ya kuchimba chakula na mashimo, Kakakuona huingiza hewa na kuongeza ubora wa virutubisho vya udongo. Hivyo kufanya ardhi kuwa na rutuba inayochochea uzalishaji wa mazao kwa ajili ya chakula cha binadamu na viumbe wengine.

Ikiwa viumbe hawa wa pekee wanafanya kila wawezalo kwa ajili ya viumbe wenzake, kwanini mimi na wewe tusishirikiane kuwalinda.

Kumbuka, VIUMBE WOTE WANA HAKI YA KUISHI.

Likes:
0 0
Views:
4613
Article Tags:
Article Categories:
HistoryTourism