Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni hifadhi ndogo kuliko zote nchini yenye eneo la kilomita za mraba 2.18.

Kisiwa hiki kinaundwa na visiwa viwili ambavyo ni chankende kubwa na ndogo na iko umbali wa takribani kilomita 1 Kusini Magharibi kutoka katikati ya Jiji la Mwanza katika ghuba ya Ziwa Victoria.

Historia ya kisiwa hiki inaleleza kuwa kilianzishwa kama bustani ya kwanza ya wanyama nchini mwaka 1964 kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya uhifadhi. Jina la hifadhi hiyo lilitokana na mwanzilishi wa bustani aliyeitwa Mzee Saanane Chawandi, aliyekuwa mwenyeji na mkazi wa kisiwa hiki.

Mwaka 1991 ikawa pori la akiba (game reserve ) na mnamo mwaka 2013 pori hili la akiba lilipewa hadhi ya kuwa Hifadhi ya Taifa.

Hifadhi hiyo ina wanyama wakipekee kama vile tumbili weusi (De-Brazza’s monkey) ambaye anapatikana pekee hifadhini hapo vilevile wapo swala, pundamilia, chatu, ndege aina mbalimbali, simba, mamba, fisi maji, samaki aina ya sato (tilapia) na samaki wengineo.

Ziwa Victoria ni sehemu ya kivutio cha hifadhi hii huku mtalii akipata fursa ya kutazama mawio ya jua na muda wa jioni ambapo ziwa hilo hutoa nafasi ya pekee kuona mandhari hii.

Shughuli za utalii zinazoweza kufanyika hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni kukwea miamba, kutazama ndege, utalii we kutembea kwa miguu, kupiga makasia kwa kutumia mitumbwi, kutalii kwa kutumia boti pamoja na uvuvi wa kimichezo (sport fishing).

Aidha, uwapo katika hifadhi hii utapata fursa ya kulala katika mahema binafsi nje ya hifadhi au kujipatia malazi nje ya hifadhi kupitia nyumba za wageni.

Likes:
0 0
Views:
1013
Article Tags:
Article Categories:
Tourism