Ifahamu Hifadhi ya Taifa ya Gombe

Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni miongoni mwa hifadhi kongwe hapa nchini Tanzania iliyosheheni vivutio mbali mbali vinavyobeba umaarufu wake. Licha ya uwepo wa hifadhi nyingine kama Mahale na Mto Ugalla zenye wanyama jamii ya sokwe lakini bado Gombe imezidi kushika hatamu kwa muda mrefu kutokana na upekee wa sokwe wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Gombe ina ukubwa wa kilomita za mraba 52 na inapatikana mkoa wa Kigoma, Magharibi mwa Tanzania ikiwa ni sehemu ya milima iliyosheheni misitu minene inayotengeneza ikolojia nzuri katika hifadhi hii.

Wanyama hawa jamii ya sokwe wanapenda kuishi maeneo ya misitu hivyo uharibifu wa misitu unaweza kuhatarisha maisha yao. Hifadhi hii inapatikana kando kando ya Ziwa Tanganyika, na uwepo wa ziwa hilo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza hadhi ya hifadhi ambapo licha ya watalii kufurahia maajabu ya sokwe wanaweza pia kufanya utalii kwa njia ya boti (boating safari).

Mnamo mwaka 1943 Gombe ilianzishwa kama pori tengefu, na mwaka 1968 ilipandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Taifa. Hifadhi hiyo imejipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na uwepo wa wanyama aina ya sokwe (chimpanzee) wanaoifanya kujulikana kote ulimwenguni na kuwa kitovu cha utalii na kupelekea kuwa na mchango mkubwaa katika pato la Taifa kwa kipindi kirefu.

Likes:
0 0
Views:
987
Article Tags:
Article Categories:
Tourism