Ifahamu Hifadhi Ya Taifa Ya Kitulo, Bustani Ya Mungu Inayopatikana Nchini Tanzania

Hifadhi ya Taifa Kitulo inapatikana Nyanda za juu Kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Mbeya na Njombe. Hifadhi hii ipo kati ya kilele cha Milima ya Kipengere, Poroto na Safu za Milima ya Livingstone. Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ina ukubwa wa kilomita za mraba 412.9. Hii ni hifadhi ya kwanza kabisa barani Afrika kuanzisha kwa lengo la kutunza mimea yake hususani jamii ya maua.

Awali hifadhi hii ilijulikana kama “Elton Plateau” baada ya kugunduliwa na Fredrick Elton aliyepita eneo hilo mwaka 1870. Baadaye mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hili na kulitumia kwa matumizi ya kilimo cha ngano na ufugaji wa kondoo.

Hata hivyo eneo hilo lilikuja kugeuzwa kuwa shamba la ng’ombe ambalo bado lipo mpaka sasa. Ila kutokana na umuhimu wa eneo hilo watu mbalimbali na wadau wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kuwa hifadhi ya Taifa ili kulinda aina mbalimbali na za kipekee za maua na mimea adimu inayopatikanakatika eneo hili.

Jitihada za kulifanya eneo hilo kuwa hifadhi ya Taifa zilianza mwaka 2002 kutangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa na serikali mwaka 2005.

Watu wengi hupendelea kuiita hifadhi hii “Bustani ya Mungu”. Hii ni kutokana na uzuri wa hifadhi hii uliopambwa na aina mbalimbali za maua mazuri yakuvutia yenye rangi nzuri na harufu za kipekee ambayo hupatikana eneo hili tu duniani kote. Wengine wameenda mbali zaidi kwa kifananisha hifadhi ya Kitulo na ile ya Serengeti. Kutokana na hilo wataalamu wa mimea wakaamua kuiita “Serengeti ya Maua” kutokana na utajiri wa aina nyingi za maua yanayopatikana hifadhini na kuifanya moja ya sehemu ya maonesho ya maua mazuri Duniani.

Hifadhi ya Kitulo ina spishi tofauti za maua zipatazo 350 ambapo aina 40 za maua haya hazipatikani popote duniani na aina 45 za okidi za ardhini ambazo huibuka na maua ya viwango tofauti wakati wa mvua kuu mwishoni mwa mwezi Novemba mpaka April kila mwaka.

Tembelea kitulo ujionee maajabu.

Likes:
0 0
Views:
1379
Article Categories:
Tourism