Kinyonga, mjusi aliyesheheni maajabu kuanzia rangi hadi mwendo

Tanzania imejaliwa viumbe vya aina mbalimbali. Mara nyingi viumbe hawa wanajulikana kwa majina na hadithi za hapa na pale tu, lakini ufahamu zaidi juu ya maisha yao unahitajika.

Leo tunamuangazia Kinyonga. Kiumbe anayesifika duniani kote kwa uwezo wake wa kubadili rangi.

Kutoka familia ya Kamilionidae, Kinyonga ni reptilia jamii ya mjusi mwenye tabia nyingi zinazomtofautisha na mijusi wengine.

Tabia moja wapo ni kubadili rangi. Ingawa watu wengi hudhani anabadilisha rangi yake ili kujifananisha na mazingira pekee, Kinyonga ana sababu nyingine nyingi zinazomchagiza kubadilisha rangi.

Kinyonga hubadilisha rangi ili kudhibiti halijoto, hutengeneza rangi nzito wakati wa baridi ili kusharabu joto na wakati wa joto huweka rangi nyepesi ili kuakisi joto. Hivyo joto la mwili wake kuendelea kuwa salama bila kuathiriwa na hali ya joto la kwenye mazingira.
Vilevile Wataalamu wa tabia za wanyama wanaainisha kuwa kubadilisha rangi ni njia mojawapo ambayo Kinyonga hutumia kufanya mawasiliano.

Kinyonga hutoa rangi nzito akiwa na msongo au hasira kama ishara ya kusema “usinisogelee,” huku rangi nyepesi za kung’aa zikiashiria siku nzuri na mvuto kwa mwenza wake. Sio hivyo tu, mabadiliko ya rangi pia yanamkinga Kinyonga dhidi ya maadui zake. Wanashindwa kumtofautisha na mazingira na wakati mwingine huchanganyikiwa na kuogopa hasa wanaposhuhudia kitendo hiko.

Je! Wajua?
Kinyonga ndiyo mnyama pekee ambaye macho yake yana uwezo wa kuangalia sehemu mbili tofauti kwa wakati mmoja.

Ni ajabu lakini ndivyo ilivyo, hata wewe hapo ulipo unaweza kujaribu.“Kwa wakati mmoja, jicho lako la kushoto liangalie kitu kilichopo mbele yako halafu jicho la kulia liangalie nyuma.”

Kwa Kinyonga hili ni jambo jepesi, wakati jicho moja linaangalia mbele lingine linaangalia nyuma, wakati moja linaangalia juu lingine linaangalia kushoto na vyote hivi anavifanya kwa wakati mmoja bila wasiwasi.

Kwa kweli kiumbe huyu haachi kuacha watu mdomo wazi kwa maumbile na uwezo wake.

Wanasayansi wamebaini kuwa Kinyonga ndio Mjusi pekee mwenye uwezo wa kuzungusha jicho lake kwa lengo la kuongeza uoni wake hadi usawa wa nyuzi 360; yaani ana uwezo wa kuona kitu kinachokuja nyuma yake bila kugeuza mwili wake.

Uwezo wa macho yake kuangalia uelekeo tofauti kwa wakati mmoja na kwa upeo wa hadi nyuzi 360 unamuongezea Kinyonga nafasi ya kujiokoa kutoka kwenye makanwa ya adui na kumfanya kuwa kivutio kwa watu wengi wanaopata fursa ya kumuona.

Je! Umewahi kujiuliza kuhusu mwendo wa kinyonga?

Kinyonga anatembea kwa mwendo wa sitaki na taka, yaani anatembea kwa kunesanesa mithili ya tawi linalopulizwa na upepo mdogo. Mwendo huu unawapotosha maadui zake na kuwafanya washindwe kumtofautisha na mazingira yanayomzunguka. Hivyo adui kama ndege wakiangaza chini kumtafuta, humuona kinyonga kama sehemu ya matawi ya miti na vichaka na kuachana nae.

Kuna mambo mengi yanayohusu maisha ya vinyonga.
Endelea kufatilia Tanzania Safari Chanel ili uweze kujua viumbe mbalimbali kwa kina zaidi.
Kumbuka Tumerithishwa, Tuwarithishe.

Likes:
0 0
Views:
1527
Article Categories:
Tourism