Maajabu ya udogo wa mchwa na ukubwa wa kichuguu

Makazi ni moja ya mahitaji muhimu ya kiumbe hai. Makazi haya yanaweza kuwa majini au nchi kavu. Baadhi ya viumbe huwa na uwezo wa kujitengenea makazi yao wakati wengine hutumia makazi yaliyotengenezwa na viumbe wengine.

Mchwa ni kiumbe mwenye umbo dogo lakini ana uwezo na utashi mkubwa wenye kushangaza wengi. Jambo mojawapo ni ujenzi wa nyumba zao kubwa na imara zinazojulikana kama vichuguu.

Vichuguu vya mchwa hujengwa kwa kutumia mate, kinyesi na udongo. Ndani ya kichuguu kunakuwa na njia nyembamba zinazowasaidia na kuwawezesha kupita pale wanapohitaji kutoka nje ya kichuguu kujitafutia chakula kama ilivyo madirisha na milango katika nyumba za binadamu.

Vichuguu hivi vinajengwa na jamii ya mchwa ambapo mchwa hushirikiana katika ujenzi bila kuwa na mchwa kiongozi. Ufundi na ustadi wa hali ya juu hutumika na hivyo kuonesha ubora wao katika usanifu na ujenzi ya vichuguu imara.

Vichuguu vinaweza kufikia urefu wa hadi mita 5 na zaidi. Wakati mwingine vichuguu hivi huchukua muda mrefu kujengwa takribani miaka mitano huku kikiendelea kufanyiwa marekebisho mara kwa mara.

Kila kiumbe kinahitaji hewa ili kupumua na kuendelea kuishi, mchwa wanalitambua hili na ndio maana wakati wa kujenga kichuguu wadudu hawa huzingatia ni kwa namna gani hewa itaingia na kutoka ndani ya kichuguu chao. Wakati wa ujenzi wa kichuguu, mchwa hutengeneza mifereji midogo midogo ambayo husaidia kupitisha hewa ndani ya kichuguu. Mifereji hii huonekana kwenye kuta za kichuguu kama matundu madogo madogo.

Lakini pia wadudu hawa hawakuishia kwenye ujenzi wa mifereji yenye kupitisha hewa, vilevile maumbo ya vichuguu hivi hutofautiana kulingana na hali ya hewa ya eneo husika.

Hii ina maana kwamba mchwa wanaopatikana maeneo ya wazi ambapo kuna joto la juu hujenga vichuguu virefu na vyenye kuta nyembamba wakati wale wanaopatikana maeneo yaliofungamana au kwenye misitu ambapo kuna joto la chini hujenga vichuguu vifupi na vyenye kuta nene. Hii husaidia kuratibu jotomwili la wadudu hawa pale wanapokuwa ndani ya kichuguu. Hivyo, kichuguu cha mchwa ni nyumba ya kisasa iliyojikamilisha.

Kweli mchwa ni msanifu stadi, usanifu huu wa vichuguu unaweza kutumiwa hata na binadamu katika ujenzi wa majengo marefu yenye kuwezesha mzunguko wa hewa ndani ya jengo.

Vichuguu vya mchwa vinaweza pia kutumika na wanyama wengine kama vile ndege na advaark.

Likes:
0 0
Views:
2160
Article Tags:
Article Categories:
Tourism