Mfahamu Mlemba, ndege mwenye mtindo wa kipekee katika malezi

Mlemba wapo kwenye jamii ya ndege wenye umbo la wastani ambao hupendelea maeneo yenye miti mingi hali inayosababisha kusikika zaidi kwa sauti zao kuliko kuonekana kwa urahisi.

Kama ilivyo kwa viumbe wengi wa angani, Mlemba wanataga mayai kwenye viota juu ya miti, lakini cha ajabu ni kuwa ndege hawa hawatamii mayai yao.

Mlemba hutaga mayai kwenye viota vya ndege wadogo hususani jamii ya ndege waimbaji (passerines) ambao ndio huishia kutamia mayai na kulisha vifaranga.

Swali linakuja Je! Hawa ndege hawajui mayai yao mpaka wakubali kulea mayai ya ndege mwingine?

Mlemba ni mwerevu, pengine baada ya majaribio ya muda mrefu ya tabia yake, mwili wa Mlemba ukaja na njia mbadala ya kumzuga mwenyeji wake.

Mlemba wanauwezo wa kutaga mayai yanayoshabihiana na mayai ya ndege mwenye kiota chake kiasi kwamba ndege huyu anashindwa kutofautisha mayai yake na ya mgeni. Lakini pia Mlemba licha ya kudhulumu kiota cha ndege wengine, huenda mbali zaidi hata kudondosha mayai ya ndege mwingine ili mayai yake yapate nafasi.

Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa hata vifaranga vya Mlemba vinapototolewa husukuma mayai ya ndege mwingine pia kwani mara nyingi mayai ya mlemba huchukua muda mchache sana kuanguliwa. Tabia hii inamwezesha mlemba kutaga kwa uhuru na kuendelea na shughuli zake bila wasiwasi kwani anasaidiwa majukumu yake ya umama na ndege mwingine.

Ndege hawa wanapatikana maeneo mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Likes:
0 0
Views:
544
Article Tags:
Article Categories:
Tourism