Mijusi, viumbe wenye damu baridi na maajabu yasiyoisha

Mijusi ni viumbe wenye damu baridi na ngozi yenye magamba kama nyoka, tofauti kubwa ya kimaumbile inayotofautisha mijusi na nyoka ni miguu. Wakati nyoka hana miguu kabisa, mjusi ana miguu minne inayomwezesha kutembea, kukimbia na kupanda miti, tafiti zinaeleza kuwa nyoka wenyewe walitokana na mijusi.

Mkia wa Mjusi sio pambo, bali una matumizi mengi yanayosaidia Mjusi kuishi vyema. Mkia unamsaidia mjusi kupata balance hasa wakati wa kutembea, kutunza mafuta (fat storage) lakini pia ni chanzo cha chakula wakati wa njaa au wakati wa kuzaliana.

Mkia pia unatumika kujikinga dhidi ya adui, pindi adui anapomkabili Mjusi huchezesha mkia wake kumtishia adui wake, lakini anapoona hali ni ngumu na adui amemkata, misuli ya mkia hujibana (constrict) kwenye sehemu dhaifu ya pingili za mkia na hatimaye kukatika. Mkia huo ukianguka huchezacheza (wiggle) na kumfanya adui kuhamishia mawazo yake kwenye mkia huo akijaribu kuukamata na kumuachia huru Mjusi hivyo hupata fursa ya kukimbia ili kuokoa maisha yake.

Mlo wa mijusi unatofautiana kulingana na mahali na aina ya mjusi husika. Mijusi wadogo hupendelea kula wadudu, ambapo humsubiri mdudu aje karibu na kisha kumnasa kwa kutumia ulimi wake mrefu. Wana meno madogomadogo yanayowawezesha kutafuna chakula chao kabla ya kumeza.

Ingawa Mijusi wote hutaga mayai, malezi kati ya mijusi hutofautiana. Spishi nyingi huchimba mashimo ambamo mayai hayo huwekwa, ilhali wengine huzika chini ya takataka za majani au huziweka kwenye nguzo za miti au mapango.

Sawa na nyoka, mjusi hutoa ulimi wake ili kukamata chembe za harufu hewani na kisha kurudisha ulimi wake na kuweka chembe hizo kwenye paa la mdomo wake, ambapo kuna chembe maalum za hisi. Mjusi anaweza kutumia “dokezo” hizi za harufu ili kutafuta chakula au mwenzi au kugundua maadui.

Mijusi wana ngozi kavu, yenye magamba ambayo haikui na miili yao. Badala yake, mijusi wengi humwaga, au huyeyusha, ngozi zao kuukuu katika madoa makubwa ili kutoa nafasi kwa ngozi mpya iliyo chini yake.

Ingawa wengi hufanya shughuli zao wakati wa mchana na kulala wakati wa usiku, baadhi ya Mijusi wanajificha mchana na kutumia usiku kucha wakiwinda chakula. Mijusi wa usiku wamebuni mifumo ya macho inayowaruhusu kusafiri vizuri gizani, huku baadhi ya mijusi wakiripotiwa kuwa nyeti sana kwa uwezo wa kuona rangi mara 350 kuliko sisi wanadamu.

Likes:
0 0
Views:
1289
Article Tags:
Article Categories:
Tourism