Mito 5 inayoipa uhai Hifadhi ya Taifa Serengeti

Ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuna mito mingi inayotiririsha maji ndani ya hifadhi na kufanya mtawanyiko wa wanyama kuwa mkubwa sana. Ifuatayo ni baadhi ya Mito inayopatikana Serengeti.

Mto Seronera

Seronera ni mto muhimu unaokatiza katikati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti hata kupelekea kanda ya kati ya hifadhi kuitwa Seronera. Mto huu Una urefu wa takribani kilomita 32.2 huku eneo la Mto Seronera likizungukwa na mapango ya mawe, matindiga na mabwawa.
Huwezi kuzungumzia Serengeti bila kuutaja Mto Seronera.

Uwepo wa maji mtoni, matindiga na mabwawa husababisha Mto Seronera kuzungukwa na Nyasi nzuri hata wakati wa masika na kuvutia makundi makubwa ya wanyama wanaokula nyasi ikiwemo Nyumbu, Pundamilia, Swala na Tembo.

Mto Seronera

Kupatikana kwa idadi kubwa ya wanyama wanaokula nyasi na mapango ya mawe karibu na mto huo inatajwa kuwa sababu ya kupatikana kwa idadi kubwa ya wanyama wanaokula nyama kama vile Simba, Chui na Duma.

Mto Grumeti

Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti, unapatikana Mto Grumeti wenye uwezo wa kukaa na maji kwa muda wa mwaka mzima, hivyo kuwavutia wanyama kutoka Kusini mwa hifadhi.

Mto huo ni kituo maarufu katika safari ya kuhama kwa nyumbu mwezi Juni kutoka Kusini kuelekea Kaskazini mwa hifadhi panapo Mto Mara.

Ni mto unaosifiwa kwa kuwa na mamba wengi ambao hupata chakula chao kwa kuwinda wanyama wanaokwenda kunywa maji au kuvuka mto.

Mto Mara

Mto mara ni mto mkubwa kuliko mito yote inayopatikana Serengeti na ndio mto maarufu duniani kote kama kivutio kikubwa katika msafara wa nyumbu.

Mto Mara unapatikana Kaskazini mwa hifadhi ukipakana na Hifadhi ya Masai Mara. Ni kilele cha safari ya kuhama kwa Nyumbu katika miezi ya Julai na Agosti. Pia mto huo ni makazi ya makundi makubwa ya Mamba ambao huneemeka kwa uwepo wa wasafiri hao wanaolaziika kupita nyumbani kwao kwenda upande wa pili, licha ya hatari wanayokutana nayo mtoni.

Mbali na ikolojia ya wanyamapori, mto huo pia ni chanzo muhimu cha maji kwa wakazi wa maeneo jirani na ni moja ya mito inayotiririsha maji yake Ziwa Victoria

Mto Mbalageti

Mbalageti ni moja ya njia muhimu katika safari ya kuhama kwa Nyumbu. Bonde la Mto Mbalageti linaunganisha tambarare na misitu na kuunda ushoroba wa asili ambao uhamiaji wa nyumbu na pundamilia hufuata kila mwaka.

Licha ya Mto Mbalageti kuwa kiungo muhimu cha safari za Nyumbu na Pundamilia, bonde la mto pia ni makazi ya Tai aina ya Martial Eagle. Ni sehemu nzuri ya kutazama Wanyama hasa wakati wa uhamiaji wa kuelekea Kaskazini na Kusini.

Mto Naironya

Mto huo unaweza kuuita Mto Ngare Naironya unapatikana uwanda wa Kaskazini Mashariki mwa Hifadhi ya Serengeti.

Mto Naironya ni moja ya mito inayotiririsha maji kwa kipindi cha masika na ifikapo kiangazi hukauka, jambo linalosababisha wanyama kuanza kusafiri kutoka uwanda wa Mashariki kuelekea ukanda wa Seronera kutafuta chakula na maji.

Umaarufu wa mito hii na uwepo wake unategemea umahiri wetu wa kuhifadhi mazingira yetu, kupanda miti, kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji na kutumia njia mbadala za nishati ili kupunguza au kurekebisha mabadiliko ya tabia nchi ambayo huchangia kwa sehemu kubwa kupotea kwa vyanzo vingi vya maji duniani. Kumbuka Maji ni Uhai.

Likes:
0 0
Views:
867
Article Categories:
Tourism