Sekta ya Utalii Tanzania ina chakujifunza kutoka Ufaransa

Ufaransa ndio taifa linaloongoza kutembelewa zaidi duniani, wengi wangedhania ni Marekani au Hispania au taifa lingine lolote barani Afrika. Lakini kulingana na Shirila la Utalii Duniani, Ufaransa ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Hispania, na Marekani ikichukua nafasi ya tatu.

Nini ambacho Afrika hasa Tanzania inaweza kujifunza kutoka taifa la Ufaransa?

Kwanza ni uzito ambao taifa hilo limeweka kwenye utalii, ambapo utalii pekee huchangia asilimia 8 ya pato la Taifa (GDP).

Ufaransa ina milima, mashamba ya zabibu za kutengeneza mvinyo, sehemu za kuvutia nyingi na pwani ndefu zenye fukwe safi na zenye kuvutia. Mashamba ya zabibu zinazotengeneza mvinyo yametunzwa kwa maelfu ya miaka na yanavutia watalii ambao baadhi yao hupata nafasi ya kuonja aina mbalimbali za mvinyo unaotengenezwa huko.

Pia, Ufaransa imetumia vizuri ramani yake ya kuwa nchi inayoweza kufikika kirahisi kutoka mataifa mengi ya bara la Ulaya, imejitengenezea mvuto unaovutia wengi bila ya sababu maalum ‘je ne sais quoi’.

Wengi wanavutiwa na Ufaransa kutokana na vyakula vya kipekee, tamaduni, uzuri wa kipekee wa nchi na mwisho ni jinsi mtu unavyojisikia unapokuwa pale. Kuna mahaba fulani ukiwa Ufaransa.

Wengi waliotembelea Ufaransa wanasema sehemu za kitalii nchini humo zinafikika kirahisi sana ukilinganisha na mataifa mengine. Ni taifa lenye mtandao mzuri wa barabara na usafiri wa umma uliopangika vizuri. Kwa hiyo kukiwa na mvua au jua unaweza kufika na kutembelewa sehemu yeyote kwa ndege au gari.

Kinachovutia hata zaidi ni kuwa wengi waliotembelea Ufaransa mara moja, hujikuta wanarudi tena na tena. Huu ni mvuto wa kipekee ukilinganisha na mataifa mengi ambayo wengi hutalii mara moja tu na hakuna cha kuwavutia kurudi tena na tena.

Tanzania inalenga kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025. Pamoja na lengo hilo, pia inaendelea kuboresha mazingira ya utalii, ili kuomgeza siku za mtalii kukaa nchini, au kumfanya arejee mara ya pili, au vyote kwa pamoja.

Ni wazi mataifa mengine, ikiwemo Tanzania, yana mengi ya kujifunza kutoka kwa taifa la Ufaransa. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwa sehemu ya kunyanyua sekta hii inayochangia sana kipato cha Taifa na sifa yake duniani.

Likes:
0 0
Views:
532
Article Tags:
Article Categories:
Tourism