Serikali yaimarisha ulinzi shamba la moyo Makere

Ikiwa ni siku 10 tangu Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma kuripoti tukio la watu wanaoaminika kuwa wafugaji kuvamia kambi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ndani ya Shamba la Miti Makere wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Prof. Dos Santos Silayo amefanya ziara kwa lengo ya kuimarisha ulinzi, usalama na kuwasaka wahusika wa tukio hilo.

Akizungumza mara baada ya kukagua na kushuhudia uharibifu mkubwa uliofanywa na wavamizi wa shamba hilo Kamishna Silayo amesema wavamizi hao wamelenga kuzuia juhudi za Serikali za kupanda na kuhifadi miti katika shamba hilo.

Amesema kufuatia hali hiyo Serikali imeimarisha ulinzi wake katika Shamba hilo na maafisa na askari waliopo eneo hilo wako tayari kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinafanyika kama ilivyokusudidwa.

“Katika tukio la uvamizi huu watendaji 2 waliuawa kikatili huku wengine 6 wakijeruhiwa vibaya,sasa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu nchini kwa kushirikiana na vyombo vyake vya ulinzi na usalama tumechukua hatua ya kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika huku tukiendea kuwatafuta wahusika wote wa tukio hili la kinyama, niwahakikishie tu, hakuna uhalifu utakaoshinda nia njema ya kuhifadhi rasilimali za Taifa.”- amesema Prof. Silayo.

Aidha, Kamishina huyo ametoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki walioguzwa na majanga ya uvamizi huu.

Septemba 5, 2022 Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu aliripoti mauaji na watu 2 na kujeruhiwa 6 pamoja na vitu mbalimbali kuteketezwa kwa moto likiwemo trekta mali ya TFS, nyumba moja ya tofali za kuchoma iliyoezekwa na bati iliyokuwa ikitumika kama ofisi, pikipiki sita za watuhumiwa waliokamatwa kwa kuingia kwenye hifadhi ya msitu kinyume cha sheria, gunia 20 za maharage, gunia 70 za mahindi, gunia 30 muhogo na gunia 20 za mtama.

Likes:
0 0
Views:
349
Article Tags:
Article Categories:
Tourism