Wizara ya Maliasili na Utalii yataja miradi ya ujirani mwema iliyotekelezwa

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zake za TAWA, TANAPA na NCAA imetekeleza miradi ya ujirani mwema kwa jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa zikiwemo Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMAs).

Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango wa Serikali kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga na Hifadhi za Taifa kwa kutoa CSR kutoka kwenye mapato yatokanayo na utalii.

“Halmashauri za Wilaya pamoja na jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa zinanufaika na mapato yanayotokana na utalii kupitia miradi mbalimbali ya kijamii inayoibuliwa na wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya (ujenzi wa majengo ya zahanati, nyumba za watumishi, ununuzi wa samani na vifaa tiba), Sekta ya elimu (ujenzi wa vyumba vya madarasa, ofisi, nyumba za walimu, vyoo, maabara, maktaba na unununuzi wa samani), Sekta ya Ujenzi (ujenzi wa barabara) na Sekta ya Maji (miundombinu ya maji)” amefafanua Masanja.

Kati ya mwaka 2009/2010 hadi 2019/2020 jumla ya miradi 182 yenye thamani ya shilingi 6,498,271,503.71 imetekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) katika halmashauri mbalimbali.

Kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kipindi cha mwaka 2016/17 – 2020/21, imepeleka jumla ya shilingi Bilioni 8.9 kwa halmashauri za wilaya 50 zinazopakana na maeneo ya hifadhi na Shilingi Bilioni 4.4 katika vijiji 61 vinavyopakana na vitalu vya uwindaji wa kitalii.

Akizungumzia eneo la Uwindaji wa Kitalii, Mhe. Masanja amesema kuwa Serikali inasaidia jamii kwa kurudisha asilimia 25 ya fedha zinazotokana na ada za wanyamapori waliowindwa katika vitalu vya uwindaji wa kitalii kwenye halmashauri zinazopakana na maeneo ya uwindaji.

Likes:
0 0
Views:
585
Article Categories:
Tourism