Ziwa Ngosi lililopo mkoani Mbeya

Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika inayozungukwa na vivutio vingi vya utalii na vingine inawezekana hata havitambuliwi na wenyeji.

Ziwa Ngosi yawezekana kuwa ni miongoni mwa vivutio hivyo.

Ziwa hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya ziwa la kreta lililopo Ethiopia linaakisi mwonekano wa bara la Afrika katika upande wa Kusini, Magharibi, Kaskazini na Mashariki.

Ziwa Ngosi linapatikana kwenye milima ya Uporoto, mkoa wa Mbeya nyanda za juu Kusini mwa Tanzania, na linatajwa kutokana na mlipuko wa volkano hivyo ni tofauti na maziwa mengine kama Ziwa Victoria au Ziwa Nyasa.

Upekee au utofauti wa ziwa hili ni kwamba ziwa hilo liko juu ya milima na katikati ya misitu na lina urefu wa kilomita 2.5, upana wake ni kilomita 1.5 , kina chake ni mita 74 na lina ukubwa wa hekta 9332.

Mwonekano wa bara la Afrika ambao upo katika ziwa la Ngosi ni sawa na mchoro unao onekana wa ramani ya bara la afrika pamoja na visiwa vyake uliopo kwenye jiwe kubwa lililopo mkoani Njombe, Kusini magharibi mwa Tanzania ambao haujachorwa na mwanadamu.

Ujazo wa maji huwa haubadiliki yani huwa hivyohivyo wakati wa masika au kiangazi.
Maajabu mengine katika ziwa hilo ni kwamba maji yake yana mwonekano wa rangi tofauti tofauti kila wakati, kuna wakati ukifika unakuta ziwa lina rangi ya samawati , kijani au nyeusi .

Ndege hupendelea kuogelea pamoja na aina fulani ya bata huwa wanaogelea humo kwa wingi na kufanya ziwa kuwa na mwonekano wa kupendeza zaidi.

Licha ya kuwa ziwa hilo linavutia kuangalia lakini halina samaki wala kuwa na historia ya uwepo wake na vilevile sio rafiki kwa kuogelea.

Kwa sasa eneo hilo linatembelewa na wageni kutoka nje ya nchi zaidi ya wenyeji na wanafunzi wa shule huwa wanafika hapo kwa wingi kwa ajili ya kujifunza.

Likes:
0 0
Views:
1426
Article Categories:
Tourism