Mtemi Mirambo, Shujaa anayeimbwa Afrika Mashariki na Kati

Jina la Mirambo ni maarufu sana hapa nchini na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Lakini pengine ni watu wachache wanaoweza kueleza Mirambo ni nani na alifanya nini kustahili hadi kuwekwa kwenye makasha ya kumbukumbu.

Fika jiji la Biashara Dar es Salaam, upo mtaa uliopewa jina lake. Tabora upo mtaa wenye jina lake, Shule ya Sekondari na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vimepewa jina la Mirambo. hii yote ni kuonyesha kwamba Mirambo hakuwa mtu wa mchezo mchezo.

Mtemi Mirambo alizaliwa mwaka 1820 eneo lililojulikana kwa jina la Ikonongo Wilaya ya Urambo (kwa sasa Kaliua) na alipewa jina la Mbula Kasanda. Baba yake mzazi na Mtemi Mirambo anaitwa Kasanda na mama yake Mwasi Mpela.

Babu yake na Mtemi Mirambo aliyejulikana kwa jina la Kasele Muhofu na ambaye aliishi zaidi ya miaka 300 alimrithisha utemi mjukuu wake Mbula Kasanda (Mirambo).

Babu yake Mtemi Mirambo, Kasela Muhofu kwa maajabu aliongea akiwa tumboni mwa mama yake kabla ya kuzaliwa na baada ya kuzaliwa hakunyonya maziwa ya mama yake.

Mbula Kasanda (Mtemi Mirambo) kabla ya kutawazwa kuwa mtemi alitanguliwa na watemi tisa wa kwanza akiwa Sibuga aliyetawala kuanzia mwaka wa 22 (Kabla ya Kristo) akafuatiwa na Mkindo wa Kwanza ambaye alirithiwa na Mlowa na kisha kufuatiwa na Moto wa Tatu.

Moto wa Tatu alirithiwa na Nsimba Nchembe ambaye naye alimwachia utawala Kapaya aliyerithiwa na Kasele Muhofu ambaye alimuachia utawala Kasimana Kasele.

Kasimana Kasele alikabidhi utawala kwa Mkindo wa Pili ambaye alimrithisha Mbula Kasanda maarufu kama “Mtemi Mirambo.”

Mtemi Milambo alianza kutawala mwaka 1838 katika eneo la Ikonongo huku akiwa na Ikulu mbili za Ikonongo na Iselamagazi.

Kabla ya kifo chake kilichotokana na homa kali, Mtemi Mirambo aliacha urithi wa kiti cha utemi kwa mtoto wake wa kike aliyejulikana kwa jina la Kibete mnamo mwaka wa 1884.

Kibete alizaliwa akiwa na titi moja la mkono wa kushoto. Kabla ya Kibete kufariki alikabidhi kiti cha utemi kwa Solomoni Kazwika Mirambo ambaye alizaliwa mwaka 1945 ambaye yupo hadi hivi sasa.

Solomoni Kazwika Mirambo kabla ya kuzaliwa aliongea akiwa tumboni mwa mama yake na hakunyonya maziwa ya mama yake pia.
Wakati anatawazwa kuwa Mtemi alitembea kwa miguu kutoka Mwanza hadi Tabora na alipofika alilala kwenye kaburi la Babu yake (Mtemi Mirambo) kwa muda siku tisa.

Koo ya Mtemi Mirambo imetoa machifu wengi na watu waliokuwa mashuhuri nchini akiwemo Bibi Titi, Mwanamalundi, Mama Mgaya (Mama Mzazi wa Mwalimu Julius Nyerere) na wengineo.

Ukoo wa Mtemi Mirambo unaendelea kurithisha utemi kizazi hadi kizazi ili kuendeleza utamaduni.

Likes:
0 0
Views:
1504
Article Tags:
Article Categories:
Uncategorized