Huyu ndiye mdudu mwenye nguvu zaidi anayeishi kwenye kinyesi

Kila siku wanyama wanakula na huzalisha kinyesi, lakini je, ni kwanini dunia haijatawaliwa na kinyesi kila mahali?

Kombamwiko au Dung Beetle kwa lugha ya kigeni, ni mdudu mwenye umbo la duara na mwenye mabawa magumu na mafupi. Mara nyingi huwa na rangi nyeusi japo wengine wanaweza kuwa na rangi nyingine.

Inasemekana, takribani asilimia 20 ya wanyama wote duniani ni wadudu kombamwiko, wadudu ambao wanaoweza kuishi katika mazingira tofauti tofauti yenye kinyesi hasa cha wanyama.

Kombamwiko wapo wa aina kuu tatu ambao ni Kombamwiko waviringishaji, Kombamwiko wajenga handaki na Kombamwiko wakazi, majina ambayo yanaelezea matumizi mbalimbali ya kinyesi kwa mdudu huyu.

Kombamwiko waviringishaji hutengeneza kinyesi na kukipa umbo la mpira kisha kukiviringisha mbali na marundo mengine ya kinyesi. Wajenga handaki hujenga mahandaki kisha kupitisha maduara ya kinyesi kwenye mahandaki hayo mpaka chini kabisa ya marundo ya kinyesi wakati Kombamwiko wakazi wao wanapendelea kuishi ndani ya marundo ya kinyesi.

Katika makala ya leo tutaangazia zaidi Kombamwiko Waviringishaji.

Kabla ya kuanza kazi ya uviringishaji ni lazima kwanza atambue mahali kilipo kinyesi. Wadudu hawa wana uwezo wa kunusa mahali kilipo kinyesi na kukifuata haraka ili kukahikikisha kila mmoja anapata fungu lake kwa sababu mamia ya kombamwiko hukusanyika katika rundo moja la kinyesi.

Kombamwiko huviringisha kinyesi kwa kutumia miguu yake ya nyuma huku yeye mwenyewe akienda kinyume nyume na kichwa chake kikiwa ardhini. Hii inaonekana kama ni kazi kubwa sana ukilinganisha na umbo la mdudu huyu, lakini husukuma miduara ya kinyesi bila kutumia nguvu nyingi.

Kama itatokea akapotea njia, basi atasimama kisha kupanda juu ya mduara wake na kutazama jua au mwezi ambao ndio unaomsaidia mdudu huyu kutambua uelekeo wake.

Si kinyesi chochote tu kinafaa kwa matumizi, Kombamwiko hupenda zaidi kinyesi cha wanyama walao majani, kama vile Tembo, Twiga na Pundamilia. Pia hupendelea kinyesi ambacho hakijameng’enywa sana na chenye maji maji ambapo Kombamwiko wakubwa hutumia majimaji hayo kama chakula.

Kombamwiko dume wana kazi kweli kweli, kwani jike hufanya uchaguzi wa dume kwa kuangalia ukubwa wa miduara ya kinyesi iliyoviringishwa na dume huyo. Hivyo dume anatakiwa kuviringirsha miduara mikubwa itakayovutia majike kwa ajili ya kuzaliana.

Je! Wajua?
Kombamwiko waviringishaji wanaweza kuvuta kitu chenye uzito mara 1,141 zaidi ya uzito wake mwenyewe. Uzito wa juu kabisa wa miduara anayoviringisha kombamwiko unaweza kufananishwa na binadamu anayesukuma mabasi manne yenye watu ndani. Hii inadhihirisha kwamba kombamwiko ni moja kati ya wadudu wenye nguvu zaidi ya wadudu wengine duniani.

Unaweza kujiuliza, Je! Kombamwiko hakuweza kupata au kutumia kitu kizuri zaidi ya kinyesi?
Jibu ni kwamba wadudu hawa wana umuhimu mkubwa sana katika maisha ya kila siku, ikiwemo kusafisha mazingira, lakini pia kutengeneza na kusambaza mbolea kwa ajili ya kurutubisha ardhi na hivyo kutengeneza ardhi yenye rutuba.

Nchini Tanzania kuna zaidi ya spishi 7,000 za Kombamwiko. Karibu Tanzania ujionee wadudu hawa wenye kushangaza.

Likes:
0 0
Views:
850
Article Categories:
Wildlife