Kiswahili na fursa za utalii Tanzania

Siku chache baada ya kishindo cha uzinduzi wa filamu ya Tanzania: The Royal Tour jijini Arusha, wanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mkoani humo wamesema kuwa utalii na Lugha ya Kiswahili vitabebana.

Wakizungumza katika kipindi cha Lulu za Kiswahili kupitia TBC1 wakufunzi hao wamesema kuwa wageni watakaokuja watajifunza lugha hiyo adhimu ambayo inazidi kukua kila uchwao barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Dkt. Neema Mturo, mhadhiri wa chuo hicho amesema kuwa Kiswahili kinaitambulisha Tanzania, hivyo ni muhimu mkazo zaidi ukawekwa katika kukikuza ili kinapoenea zaidi duniani Tanzania izidi kutambulika pamoja na vivutio vilivyopo.

Kwa upande wake Dkt. Joachim Kisanji amesema kuwa utalii utakuza lugha hiyo kwani watalii watakapokuja nchini watajifunza maneno kadhaa ya lugha hiyo na wanapoondoka wataondoka nayo, hivyo hiyo ni njia moja ya kuikuza.

Baadhi ya wanafunzi waliotoa maoni yao wamehimiza suala la uzalendo kwa wadau wote wa utalii kwa wao kuwahudumia watalii kwa viwango vya juu, ili kukuza sekta hiyo zaidi na Lugha ya Kiswahili.

Likes:
0 0
Views:
2085
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife