Maajabu ya mnyama Mhanga porini

Kichwa kirefu chenye pua ndefu iliyochomoza, kucha zilizotengenezwa kwa ajili ya kuchimba na miguu iliyoimara ndio kati ya sifa zinazomfanya mnyama huyu ajikite zaidi katika ulaji wa wadudu. Miguu yake hailingani, miguu ya nyuma ni mirefu kuliko miguu yake ya mbele.

Mhanga ni mnyama mwenye ukubwa wa kati na uzito wa kuanzia kilogramu 40 mpaka 80. Ni mnyama mwenye aibu, mwenye kufanya shughuli zake hasa nyakati za usiku na huonekana kwa nadra sana. Mashimo na mikwaruzo yake huonekana kwa urahisi zaidi ya mnyama mwenyewe.

Mhanga ni mnyama anayepatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara hasa katika maeneo yenye idadi kubwa ya mchwa na siafu pamoja na lava wa Kombamwiko. Pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kuchimba mashimo marefu tena kwa haraka, wanyama hawa mara nyingi huepuka maeneo yenye udongo mgumu au wenye mawe pamoja na maeneo yanayokumbwa na mafuriko.

Kucha zake zenye kufanana na sepeto ndio nyenzo muhimu inayotumika katika kupasua vichuguu vya mchwa na kuchimba mashimo yenye urefu unaoweza kufika takriban mita 6 na milango mingi ambayo hutumika kama maeneo ya kupumzika, kujificha dhidi ya maadui na hata kulelea watoto wao. Katika maeneo yenye udongo rafiki, Mhanga hutumia nguvu kiasi na kasi katika kuchimba mashimo yao. Inasemekana, anaweza kuchimba mita moja ndani ya sekunde 15.

Mhanga anaweza kutelekeza shimo lake na likatumika na wanyama wengine kama vile reptilia, mamalia na ndege wa aina mbalimbali. Nungunungu na fisi wanaweza kufanya marekebisho kidogo katika mashimo na kuyatumia kwa matumizi yao binafsi. Mbwa mwitu nao wamewahi kuonekana kutumia mashimo ya Mhanga katika kuficha watoto wao. Mara nyingi tabia ya kutelekeza mashimo hufanywa na madume huku majike wakipendelea zaidi kutumia shimo moja kwa muda mrefu.

Mlo wake mkubwa ni wadudu aina ya mchwa, hivyo nyakati za usiku hutoka katika mashimo yao na kuanza kuzunguka huku na kule umbali wa kuanzia kilomita 10 mpaka 30, kutoka katika kichuguu kimoja mpaka kingine ambapo hukamata mchwa akitumia ulimi wake mrefu wenye kufikia sentimita 30 uliojaa mate mazito na yenye kunata unaomsaidia kunasa mchwa. Uwezo mkubwa wa kunusa unamsaidia kunasa hata mchwa walio nje ya kichuguu.

Wanyama hawa wanapendelea sana kujitenga yaani kuishi mmoja mmoja, dume na jike wanakutana katika kipindi cha kuzaliana tu. Baada ya miezi 7 mtoto mmoja tu huzaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 2 na tayari akiwa na kucha zilizokuwa vizuri.

Mtoto ataendelea kukaa shimoni kwa muda wa wiki mbili, kisha atamfuata mama. Ndani ya wiki 14 anaanza kula mchwa na baada ya wiki 16 ataacha kunyonya. Mtoto anaanza kuchimba mashimo yake mwenyewe mara anapotimiza umri wa miezi 6 na atamuacha mama yake hata kabla hajatimiza mwaka mmoja.

Mhanga ni mnyama muhimu sana katika ikolojia ya wanyamapori, kitaalamu anajulikana kama “Keystone species”. Hii ina maana kwamba mfumo wa maisha yake unawezesha au kurahishisha maisha ya viumbe wengine kama vile ndege, reptilia na mamalia wengine ambao hutumia mashimo ya Mhanga kujificha au kuficha watoto wao dhidi ya maadui.

Likes:
0 0
Views:
1681
Article Categories:
TourismWildlife