Machache ya kufahamu kuhusu Twiga

Twiga ni mnyama mrefu kuliko wote waishio ardhini.

Wanyama wenzake wanaokula majani kama vile Pundamilia na Swala hujisikia amani kukaa naye kwa kuwa huona hatari tangu ikiwa mbali na urefu wake hata binadamu anaweza kupita katikati ya miguu ya twiga kijana bila kugusa mwili wake, na bado ikabakia nafasi kubwa juu kwani Twiga ana urefu wa kati ya mita 4.8 na 5.5.

Mnyama huyu ni mpole na anatembea kwa madaha lakini licha ya upole wake Teke lake likimpata binadamu uwezekano wa kupona ni mdogo, hata wanyama wanaomuwinda huliepuka teke hilo ambapo Miguu ya mbele ndiyo huitumia sana kama silaha yake wakati wa mapigano na ya nyuma hutumia inapobidi kama anapambana na mnyama zaidi ya mmoja ila ni nadra.

Twiga hubeba mimba takriban siku 400 hadi 460 , ambazo ni sawa na miezi 14 hadi 15, ambapo mara nyingi huzaa ndama mmoja, huku mapacha ni nadra.

Mama hujifungua akiwa amesimama na kondo lake hukatika mara moja mtoto aangukapo ardhini tofauti na wanyama wengine kama vile Ng’ombe huchukua saa kadhaa kondo kudondoka.

Urefu wa ulimi wake ni kati ya sentimeta 46 hadi 50.

Mnyama huyu anapatikana katika nyika hususan sehemu zenye miti ya Migunga na Mikakaya ambayo huifurahia sana kwani ndio chakula chake kikuu na wana uwezo wa kukimbia takriban kilometa 55 kwa saa.

Twiga hao wanapatikana Iringa kwenye Pori Tengefu la Lunda linalopakana na hifadhi ya Ruaha, pori hilo linajulikana kama Mbomipa ikiwa ni kifupi cha Matumizi Bora ya Malihai Idodi na Pawaga.

Likes:
0 0
Views:
661
Article Categories:
Wildlife