Maelezo ya ya uwepo wa Nyati weupe Hifadhi ya Tarangire

Na Dkt. Julius Keyyu

Hivi karibuni mijadala iliibuka baada ya kuonekana kwa Nyati weupe (white and cream coloured buffalo) katika Hifadhi ya Taifa Tarangire. Miongoni mwa yaliyozungumzwa ilikuwa ni nini kinasababisha mnyama huyo kuwa mweupe tofauti na mazoea kwamba nyati huwa weusi.

Mwonekano (kwa macho na picha) na viashiria vya awali (phenotypic manifestation) vinaonesha kuwa nyati hawa wana tatizo la albino (albinism).

Hata hivyo kuonekana kwa nyati wawili wenye albino ndani ya wiki moja katika hifadhi moja wakati albino katika wanyama wenye uti wa mgongo (vertebrates) ni tukio la nadra (rare event) linaleta maswali mengi na hivyo kuhitaji utafiti wa kina.

Albinism ni tukio linalotokea kwa mnyama mmoja kati ya wanyama 20,000 hadi milioni moja. Hivyo ni mara chache kutokea. Kwa ujumla, tatizo la albino kwa wanyama limeshaonekana kwa wanyama zaidi ya aina (species) 572 duniani.

Tatizo la albino kwa wanyama linaweza kuwa albino kamili (true albinism) au albino nusu (partial albinism).

Ualbino unasababishwa na mambo mengi ikiwemo kurithi (inheritance), tatizo katika vinasaba (genetic mutations), vyakula, mazingira (living condition), umri, ugonjwa, nk.

Ili kujiridhisha na matukio haya mawili ndani ya wiki moja, na kwa nini hawa nyati wako hivi, na kama ni albino au la; Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
imetuma watafiti wake kuwafuatilia nyati hawa kwa kina, ikiwemo kukusanya taarita zao, historia yao, na kuchukua sampuli ili kujiridhisha kama hawa nyati ni albino au la.

Watafiti pia watawafuatilia nyati hawa kwa karibu na kwa muda mrefu ili kujua maendeleo yao, ikiwemo kuwafunga miranda ya mawasiliano ili kurahisisha ufuatiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Likes:
0 0
Views:
1028
Article Categories:
TourismWildlife