Maisha ya Fisi katika hifadhi za Tanzania

Fisi mnyama anayesifika kote duniani kwa sifa yake ya ukorofi na kula mizoga. Tanzania ina aina mbili za Fisi; Fisi madoa na Fisi maji. Fisi hawa wanatofautiana kidogo hasa kimaumbile na mwonekano.

Fisi maji ana mwili mdogo kuliko Fisi madoa huku rangi yake ikiwa ni kijivu yenye mistari meusi wakati Fisi madoa ana rangi ya kahawia yenye vidoti vyeusi. Rangi ya Fisi ni silaha kwake kwani humfanya asionekane kwa urahisi kwa sababu nyasi nazo huwa na rangi ya kahawia hususani kipindi cha kiangazi.

Tofauti na wanyama wengi, miguu ya mbele ya Fisi ni mirefu kuliko miguu ya nyuma na pengine hali hii inamsaidia Fisi kuwa imara kupambana na maadui au hata kuwatisha kwa umbile lake.

Fisi jike ni mkuu kuliko dume.
Fisi jike ni mkubwa, mkali na shupavu katika kulinda makazi na hata kugombania chakula kuliko dume na hii huwa ni ishara ya kwamba jike ndio kiongozi na mwenye mamlaka kuliko dume.

Fisi madoa hupendelea kukaa kwenye makundi ambapo, kundi linaongozwa na jike mmoja huku wengine wakitii na kufuata amri za jike huyo, yaani jike huyo akiamua kuwinda basi na wengine wanawinda na akiamua kupumzika na wao wanapumzika.

Vilevile jike anayeongoza kundi la Fisi ndiye mwenye mamlaka makubwa ya kuzaa ingawa imerekodiwa hata majike wengine wanaruhusiwa na jike mwongoza kundi kuzaa.

Watoto wa Fisi huuwana wao kwa wao
Fisi anapopata mimba anaibeba kwa takribani miezi minne na kuzaa watoto wawili au watatu (ingawa ni nadra sana kushuhudia Fisi akizaa watoto watatu)
Tofauti na wachanga kutoka kwa wanyama wengine wanaokula nyama, watoto wa fisi wenye madoadoa huzaliwa wakiwa na meno tayari na uoni mzuri.

Mama anapozaa mapacha, ndugu hao wawili hushiriki katika majibizano makali ili kudhibiti upatikanaji wa maziwa ya mama mara baada ya kuzaliwa. Aliyedhaifu huweza kupoteza maisha au la huishia kuwa mnyonge kwa ndugu yake.

Baada ya kufikisha umri wa miaka miwili, madume yaliyolelewa yanafukuzwa katika kundi na kwenda kuanza maisha yao, huku majike yakiendelea kubaki kundini.
Taya la fisi ni imara zaidi ya Wanyama wengine wanaokula nyama.

Fisi anasifika na kutambulika kama mnyama mwenye meno imara na makali yanayomfanya aweze kula mzoga na hadi kutafuna mifupa.

Chakula kikubwa cha Fisi ni mizoga kwani inarekodiwa asilimia 40 ya chakula anachokula ni mizoga ya wanyama wenye kwato mfano Swala, Nyumbu, Swala tomi na Swala granti.

Wakati mwingine Fisi hula chakula zaidi ya kipimo. Mara baada ya Fisi kuvimbiwa hujiviringisha kwenye tope kwa lengo la kurahisisha na kuharakisha mmeng’enyo wa chakula. Hivyo kumuondolea adha ya mahangaiko.

Fisi ni mjanja sana, shupavuu na mnyama asiyekata tamaa. Hivyo hata akute Simba kakamata kitoweo Fisi anatumia ushupavu wake, ujanja wake na wingi wao katika kundi kumfukuza Simba na hivyo kula kitoweo kile.

Na ikiwa Simba atakaidi kuondoka na kuacha windo lake, hapa ndio vita inaposhamiri na hatari yaweza kumkuta Simba kwa sababu wingi wa Fisi ni hatari kwa uhai wake.
Ndani ya hifadhi nyingi hapa Tanzania, Fisi wanapatikana kwa idadi kubwa kuliko wanyama kama Simba, Chui, Duma na Mbwa mwitu.

Likes:
0 0
Views:
2285
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife