Mbwa mwitu wa Afrika

Mbwa Mwitu ni mnyama mwenye umbo lenye kufanana na mbwa wa kufugwa mwenye uzito wa kilogramu 18 mpaka 36. Mpangilio wa rangi za mwili wake ni wa kipekee na hutofautiana kati ya mbwa mwitu mmoja na mwingine. Mbwa mwitu ana miguu mirefu yenye vidole vinne, tofauti na mbwa wengine wenye vidole vitano katika miguu yao ya mbele. 

Wanyama hawa huishi katika kundi la mbwa mwitu sita mpaka 20 linaloongozwa na mbwa dume na jike ambao huwa kama baba na mama wa familia. Mbwa jike anaweza kuzaa watoto wawili mpaka 20 ambao hulelewa na familia nzima. 

Mbwa mwitu amejikita zaidi katika uwindaji wa Wanyama jamii ya Swala ambao uzito wao hauzidi mara mbili ya uzito wa mbwa mwitu mwenyewe. 

Baadhi ya makundi ya mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti yamejikita zaidi katika kuwinda Pundamilia wenye uzito wa mpaka kilogramu 240 (Malcolm, J. R. & Van Lawick, H. (1975). “Notes on wild dogs (Lycaon pictus) hunting zebras”.

Aina yake ya uwindaji ni tofauti na wawindaji wengine kwani mbwa mwitu humkimbiza manyama huku akimchomoa nyama za pembeni kidogo kidogo kwa kumng’ata mpaka mnyama atakapoishiwa nguvu kabisa na kuacha kukimbia. Uwindaji huu hufanywa na kundi zima la mbwa mwitu. 

Mafanikio ya mbwa mwitu katika uwindaji yanategemea vitu vitatu; Mazingira ambapo uwindaji huo unafanyika, aina ya mnyama anayewindwa na hata ukubwa wa kundi husika linalowinda, lakini mbwa mwitu wa Afrika uwindaji wake ni wa mafanikio zaidi: asilimia 60 mpaka 90 ya uwindaji wao huishia na kupata kitoweo. Wanyama wadogo kama vile sungura na ndege huwindwa na mbwa mwitu mmoja na si kundi kama ilivyo kwa wanyama wakubwa. 

Mbwa mwitu anatabia ya kula haraka, kundi moja linaweza kumaliza Swala Tomi mmoja ndani ya dakika 15. Kundi moja la mbwa 17 mpaka 43 limewahi kurekodiwa kuua wastani wa wanyama watatu kwa siku. 

Katika kipindi cha mvua, Watoto wa mbwa mwitu huzaliwa na kufichwa katika mashimo yaliyojengwa na Mhanga au Nungunungu. Baada ya mwezi mmoja, Watoto hutoka kwenye mashimo na kuanza kula nyama kidogo zinazoletwa na mbwa mwitu wengine katika familia yao.

Watoto hao watakuwa tayari kufuata msafara wa mbwa mwitu wengine pale tu wanapotimiza umri wa wiki 9 na watakuwa mbwa mwitu wakubwa ndani ya mwaka 1.  

Jambo la kusikitisha ni kwamba, Shirika la Uhifadhi ya IUCN limemuorodhesha mbwa mwitu kuwa ni kati ya wanyama waliohatarini kutoweka, hali inayosababishwa na magonjwa, uwindaji wa wanyamapori pamoja na kukosekana kwa makazi ya wanyama hawa kutokana na ongezeko la binadamu na shughuli za kibinadamu.

Hifadhi ya Taifa Serengeti na hifadhi zilizo Kusini mwa Tanzania ni kati ya maeneo machache ambayo yamesalia kuwa maskani muhimu kwa wanyama hawa. 

Likes:
0 0
Views:
1077
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife