Mfahamu Mnyama mkubwa kuliko wote duniani

Mpaka hivi sasa hakuna mnyama aliyetambulika kuwa mnyama mkubwa kumzidi Nyangumi wa bluu (Blue Whale), hivyo anaaminika kuwa ndiye mnyama mkubwa anayeishi katika uso wa dunia.

Nyangumi huyu ni mamalia mwenye mwili mrefu na rangi ya bluu inayoonekana vizuri anapokuwa ndani ya maji. Mnyama huyu anatawala bahari akiwa na urefu wa mita 30 na uzito wa kilogramu 180,000.

Nyangumi wa bluu mara chache huonekana wakiogelea katika makundi madogo lakini mara nyingi huonekana mmoja mmoja au wawili wawili. Katika majira ya joto, nyangumi hupatikana kwa wingi katika bahari zilizo karibu na ncha ya Kaskazini na kuhama kurudi bahari zilizo karibu na ikweta wakati wa kipindi cha majira ya baridi japo njia zao hazijafahamika vizuri.

Mnyama huyu anaweza kuogelea katika mwendokasi wa kilomita 8 kwa saa wakati wa kula au kusafiri, japo anaweza kufika mpaka kilomita 32 kwa saa kwa safari fupi.

Mbali na kuwa na sifa ya kuwa mnyama mkubwa kuliko wote duniani, nyangumi wa bluu pia ana sifa ya kuwa moja kati ya wanyama wenye uwezo wa kutoa sauti kali ambayo iwapo mazingira ya bahari yakiwa rafiki basi sauti hiyo inaweza kusikika na nyangumi wengine walio umbali wa kilomita 1,600. Wanasayansi wanadai kuwa nyangumi hutumia sauti hizo kuwasiliana.

Pamoja na Nyangumi kuwa ni mnyama mkubwa kuwahi kuishi duniani lakini mlo wao mkubwa unakamilishwa na viumbe wadogo wa baharini aina ya krill, japo pia anaweza kula samaki na viumbe wengine wa bahari.

Inasemekana ulimi wa nyangumi unaweza kuwa na uzito sawa na uzito wa mnyama tembo, lakini moyo wake pia unaweza kufikia uzito wa gari.
Nyangumi jike hubeba mimba kwa muda wa miezi 11 mpaka 12 na kuzaa mtoto mmoja tu kila baada ya miaka mitatu. Mtoto wa nyangumi wa bluu huzaliwa akiwa tayari ameorodheshwa kuwa miongoni mwa wanyama wakubwa duniani kwani huzaliwa akiwa na uzito wa kufikia kilogramu 3,000 na urefu wa mita 8.

Mtoto huyu hunyonya lita 600 za maziwa kila siku akiwa ndani ya maji, na kuongeza takribani kilogramu 90 kila siku katika mwaka wake wa kwanza. Nyangumi wa bluu anaweza kuishi mpaka kufikia umri wa miaka 80 mpaka 90.

Shirika la Uhifadhi la IUCN linamuorodhesha Nyangumi wa Bluu kuwa ni mnyama aliyehatarini kupotea. Kwa sasa, Inakadiriwa idadi ya Nyangumi wa bluu kuwa ni kati ya Nyangumi 10,000 mpaka 25,000.

Mnyama huyu anapatikana katika bahari mbalimbali duniani ikiwemo Bahari ya Hindi.

Likes:
0 0
Views:
61
Article Categories:
TourismWildlife