MJUE NDEGE KARANI MWINDAJI WA NYOKA

Je, Unamfahamu ndege anayejulikana kama ndege Karani au Secretary bird kwa lugha ya kigeni? 

Ndege Karani anapatikana maeneo ya uwanda wa nyasi ambapo huonekana akiwa anatembea huku na huko akijitafutia chakula licha ya kuwa mpaaji mzuri.

Mara nyingi ndege hupewa majina kwa kufuata maumbo yao, rangi za manyoya au tabia zao, vivyo hivyo kwa ndege karani pia ambaye nae amepewa jina hili la karani sababu ya rangi za manyoya pamoja na muonekano wake. 

Mwili wa ndege Karani umefunikwa kwa manyoya ya rangi ya kijivu huku ncha ya mkia wake mrefu ukiwa na rangi nyeusi. Juu ya kichwa cha ndege Karani kuna manyoya ya rangi nyeusi yenye kuchanua yanayomfanya kuwa na muonekano wa kuvutia mithili ya makarani wa zamani waliokuwa wakiweka kalamu katika masikio yao bila kusahau kujistiri kwa makoti ya rangi ya kijivu na suruali nyeusi ambayo yaliongeza unadhifu Zaidi; mpangilio huo unasadifu sana jina la Ndege Karani!

Chakula kikuu cha ndege Karani ni wanyama kama vile panya, wadudu na reptilia aina ya mijusi na nyoka, hivyo Karani huyu wa pori amelazimika kuwa mwindaji Hodari ili kumfukuzia mbali adui Njaa. 

Pengine Ndege karani alimsikia mhenga aliyesema Mgaagaa na upwa hali wali mkavu, kwani Ndege huyu anaweza kumaliza hadi kilomita 32 akizunguka huku na huko kwenye uwanda wa nyasi kuwinda wanyama kwa ajili ya chakula. 

Ndege karani ni maarufu na mahiri sana katika uwindaji wa nyoka wa aina mbalimbali huku akitumia miguu yake kama silaha katika uwindaji. Mbali na uwindaji wa ardhini unaofanywa na ndege karani kumtofautisha na ndege wengine wawindaji ambao huwinda wakitokea angani, ndege Karani ana miguu mirefu ambayo ni tofauti kabisa na miguu ya wawindaji wengine. 

Weledi na umahiri wa karani huyu juu ya kuwinda na kula nyoka unatokana na uwepo wa kucha kali na magamba katika miguu yake hivyo kumsaidia kukamata Nyoka wa aina mbalimbali kwa kuwakanyaga kwa nguvu na kwa haraka huku akimjeruhi kwa kucha zake mpaka atakapokufa kisha kummeza mzima mzima. 

Unaweza kujiuliza je, ni kwa namna gani ndege huyu anaweza kuwinda nyoka na wakati mwingine nyoka hatari na wenye sumu bila yeye mwenyewe kudhurika kwa kung’atwa na nyoka hao?

Karani ni mjanja na makini sana, Endapo nyoka atajaribu kumng’ata ndege karani basi nyoka huyo ataishia kubaki na manyoya tuu kwa sababu magamba yaliyopo kwenye miguu yake huongeza ulinzi dhidi ya kung’atwa na nyoka wakati wa mawindo. 

Ndege karani anapendelea kujenga viota juu ya miti hasa miti aina ya migunga. Viota hivi hujengwa kwa kutumia vijiti, matawi, majani, manyoya ya wanyama na kinyesi. Mara nyingi kiota kikishajengwa kinaweza kutumika kwa miaka kadhaa huku kikifanyiwa marekebisho madogo madogo. 

Ndege huyu anataga yai moja hadi mayai matatu na kuyaatamia kwa muda wa takriban siku 50 na katika kipindi hiki chote, si dume wala jike bali wote wanashirikiana kwa pamoja katika kuatamia na kuhakikisha usalama wa mayai na upatikanaji wa chakula hadi mayai yanapototolewa. 

Ni ushujaa, upendo na hamasa ya kuhakikisha vifaranga vinavyopatikana vinaishi hadi inapofika muda wakujitegemea 

Tembelea hifadhi za Taifa nchini Tanzania ujionee uzuri na uhalisia wa ndege karani. 

TUMERITHISHWA TUWARITHISHE.

Likes:
0 0
Views:
956
Article Categories:
Wildlife