Mondo, mnyama jamii ya paka

Mondo, mnyama jamii ya paka mwenye maumbile tofauti na paka wenzake

Mondo ni miongoni mwa jamii ya Paka wadogo ambaye sawa na Paka wengi yeye pia hula nyama na ni mwindaji mahiri akiwa porini.

Tofauti na Paka wengine, ni rahisi sana kumtambua Mondo kutokana na upekee wake wa maumbile.

Miguu ya Mondo ni mirefu sana huku kichwa chake kidogo kikishikiliwa na shingo ndefu ukilinganisha na umbo lake hata kusababisha kupewa jina la utani “Paka-twiga”. Maumbile haya yanamtofautisha Mondo na jamii zote za Paka wa nyikani au nyumbani.

Mbali na miguu mirefu, upekee wa Mondo unajidhihirisha pia kwenye masikio yake.
Ana masikio marefu kuliko Paka wengine ukilinganisha na ukubwa wa kichwa chake.

Muundo huu wa masikio unaelezwa kuchochewa na mazingira yake ya uwindaji ambapo, mara nyingi mnyama huyu huwinda Panya na wanyama wadogo wanaopatikana kwenye ukanda wa nyasi. Nyasi zinapokuwa ndefu sana humzuia kuona windo lake kwa urahisi hivyo hutegemea zaidi mawimbi ya sauti ili kupata uelekeo wa kitoweo chake.Kwa sababu hiyo akiwinda hufinya macho yake huku akisimamisha masikio yake marefu kunasa mawimbi ya sauti.

Mnyama huyu wa mdogo na wa kuvutia anapatikana maeneo mbalimbali nchini Tanzania na amevutia watu wengi kwa rangi yake ya dhahabu na nyeusi.

Likes:
0 0
Views:
1141
Article Tags:
Article Categories:
Wildlife