Serikali kuongeza Nguvu kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu

Serikali imesema kuwa itaendelea kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ili wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya Hifadhi wanufaike na maeneo hayo kwa kuendesha shughuli za utalii badala ya kulima mazao yanayopendwa na wanyamapori hao.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Arusha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka wakati wa Kikao cha Kamati Tendaji ya Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara

Prof. Sedoyeka amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti katika kuhakikisha kuwa migongano kati ya binadamu na wanyamapori inadhibitiwa kabla ya kuleta madhara ili wananchi waweze kufurahia uwepo wa wanyamapori.

” Tunataka kuona migongano baina ya binadamu na wanyamapori inapungua ili wananchi wazidi kutoa ushirikiano katika kuimarisha ulinzi wa wanyamapori wakubwa wakiwemo tembo na faru ambao wapo hatarini kutoweka” Amesema Prof. Sedoyeka

Amesema wananchi wakinufaika na shughuli za uhifadhi watakuwa mstari wa mbele katika kuwafichua majangili kabla hawajawadhuru wanyamapori, hivyo Wizara inafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha wanyamapori wakali na waharibifu hawaathiri maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine , Prof.Sedoyeka ametoa onyo kwa wananchi waache kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima katika mapito ya wanyamapori ili kuepuka kupata hasara.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kikao cha nne cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kuzuia na Kupambana na Ujangili na Bashara haramu ya nyara , Christine Musisi amesema suala la kupunguza migongano kati ya Binadamu na Wanyamapori linahitaji ushirikiano baina ya Serikali na wananchi wanaoishi katika maeneo karibu na Hifadhi.

Likes:
0 0
Views:
436
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife