Umaarufu wa Michoro ya Pahi

Moja kati ya vitu vinavyoitambulisha Kondoa Irangi duniani, ni upekee wa michoro kwenye miamba inayopatikana kijiji cha Pahi.

Michoro ya Miambani Pahi, inasadikiwa kuchorwa kati ya miaka 100 hadi miaka 10,000 iliyopita na watu wa jamii za wawindaji, wafugaji, wakulima na wakusanyaji.

Michoro hii imegawanyika kwenye makundi mawili michoro mekundu na njano na ile meupe na nyeusi.

Michoro mekundu ndio yenye umri mrefu zaidi ikikadiriwa kuchorwa miaka takribani 5,000 iliyopita.

Hii ilichorwa kwa kutumia mchanganyiko wa mwamba mlaini unaojulikana kama oka ambao husagwa na unga wake kuchanganywa na kimiminika cha mti wa Mkuyu na mafuta ya mnyama jamii ya swala na kisha kutumika kuchora kwa kutumia mwiba wa Nungunungu kama brashi.

Michoro meupe na meusi husadikiwa kuwa na umri wa miaka takribani 3000 na imechorwa kwa kutumia mchanganyiko wa majivu kwa rangi nyeupe, mkaa kwa nyeusi, kinyesi cha ndege na mafuta ya mnyama jamii ya swala na kuchorwa kwa vidole.

Jamii inayohusishwa na michoro hii ya awali ni ile ya Wasandawe ikiwa ni njia ya mawasiliano, simulizi pamoja na kutunza historia kwa kipindi hicho.

Kwa sasa michoro hii imeiweka Tanzania kwenye moja ya vivutio vya Urithi wa Utamaduni Duniani chini ya UNESCO tangu mwaka 2006 na kuwa chanzo cha kipato, sehemu ya mafunzo kwa vitendo na pia kuonesha historia ya nchi.

Kwa Afrika Pahi inaongoza kwa michoro yenye umri mrefu zaidi ila kwa dunia inaongoza kuwa na michoro mingi zaidi ndani ya eneo moja ikiwa ndani ya Pahi mawe zaidi ya 1000 yamechorwa.

Ama kwa hakika, upekee wa michoro hii ya miambani Pahi, unafanya kivutio hiki kuwa urithi unaoishi kwa karne na karne.

Likes:
0 0
Views:
579
Article Categories:
HistoryTourismWildlife