Urafiki wenye faida wa Mamba na Kiboko

Hapo awali, kulikuwa na viboko na mamba kwa wingi kote barani Afrika. Hata hivyo, kutokana na shughuli za binadamu, Mamba na Viboko wanalazimika kuishi katika maji ya kina kifupi pamoja.

Viboko ni wanyama walao majani na wanahitaji kiasi kikubwa cha nyasi (takribani kilogramu 68 kwa siku) ili kujiendeleza. Kwa upande mwingine Mamba ni wanyama walao nyama na watakula samaki pamoja na wanyama walao nyasi wanaoshuka kunywa maji. Kwa hivyo, mamba ni wanyama wanaowinda wanyama wengine na viboko ni mawindo ya kweli, cha kushangaza wanyama hawa wawili hukaa pamoja bila wasiwasi wowote. Kwa nini?

Ukweli ni kwamba akipewa nafasi mamba angemvamia na kumla kiboko lakini hawafanyi hivyo kwa sababu ya hatari ya Kiboko. Kiboko aliyekomaa anahitaji tu kuufungua mdomo wake hadi usawa wa nyuzi 180 na kufichua meno yake ya kutisha yaliyoshikiliwa na taya zenye nguvu tayari kuuma au kuvunja yeyote na chochote kinachokuja njia yake. Hali hii inasababisa Mamba kuepuka vita na Kiboko akihofia maisha yake.

Vilevile ukubwa wa Kiboko na ngozi ngumu si shabaha rahisi kwa Mamba. Mamba mwenye ukubwa wa wastani hafananishwi na Kiboko aliyekomaa wa ukubwa wa wastani hivyo mamba huepuka kutumia nguvu nyingi sana kuwinda ilhali mafanikio ni kidogo sana . Ingawa Mamba wanaweza kumudu kukamata watoto wa Viboko, ni nadra sana kufanya hivyo kwa vile viboko huishi katika makundi. Mamba huogopa kufata hao watoto wakihofia kipigo kutoka kwa viboko wakubwa.

Je! Ni uhusiano huu unawanufaisha vipi Viboko?

Viboko huwa na ushindani kutoka kwa walaji wengine wa mimea kama Pundamilia, Kongoni na hata Nyumbu. Wanyama wote wanaokula mimea kwa kawaida hutumia chakula karibu na ziwa au bwawa kisha kunywa maji, jambo ambalo husababisha kupungua kwa chakula cha Kiboko katika maeneo ya hayo na kulazimu Viboko kutembea umbali mrefu kutafuta chakula wakati wa jioni na usiku.

Hata hivyo, Mamba akiwa jirani, walaji hawa majani huwa wanaogopa. Hofu hii inawaweka mbali na maeneo ya ziwa au bwawa na kuwapa Viboko nafasi nzuri ya kupata chakula kingi kadiri wawezavyo karibu na maskani yao ya majini. Kwa maneno mengine, Mamba huwinda na kuwatisha wanyama wengine wanaokula mimea na kuacha mimea yote kwa ajili ya Kiboko pekee. Ni kama rafiki mzuri.

Je! Uhusiano huu unawanufaisha vipi Mamba?

Mwonekano uliotulia wa Viboko huwavutia walaji wengine wa mimea karibu na ziwa au bwawa, hasa kunywa maji wakidhania ni eneo salama wasijue tayari Mamba wanawapigia mahesabu. Pindi wanapoinama kunywa maji, Mamba bila kuchelewa huwakamata na kuwafanya chakula.

Licha ya wanyama hawa kuishi kwa amani pamoja kwenye maji, migogoro na mikwaruzano ya hapa na pale hutokea hasa pale ambapo mnyama mmoja hujaribu kuingilia himaya ya mwingine, lakini hilo halisababishi Mamba na Viboko kutambuliwa kama maadui.

Likes:
0 0
Views:
1117
Article Categories:
Wildlife