Mfahamu Nyuki na Tabia zake

“Fuata Nyuki ule asali”, Ni msemo uliozoeleka sana kutokana na tabia ya Nyuki kutengeneza asali tamu inayotumika kama chakula na dawa.

Zifuatazo ni tabia za Nyuki.

Nyuki anatoka familia moja na Nyigu

Nyuki ni wadudu wadogo wanaotoka kwenye jamii moja na Nyigu inayofahamika kitaalam kama Hymenoptera, Wadudu hawa wanasifika kwa kuwa na maumbo madogo yaliyogawanyika vyema katika vipengele vitatu yani kichwa, kifua na tumbo huku tumbo na kifua vikigawanyishwa kwa kiuno chembamba hata kuwapa wadudu hawa muonekano wa kuvutia.

Sio Nyuki wote huishi kwa koloni.

Imezoeleka mara nyingi kuona nyuki wakiwa kwenye makoloni makubwa. Lakini ukweli ni kuwa Nyuki wamegawanyika katika aina kuu mbili, aina ya kwanza ni Nyuki wanaopendelea kuishi maisha ya upweke yaani solitary na aina ya pili ni nyuki wanaopendelea kukaa maelfu kwa maelfu kwenye koloni moja.

Nyuki wana mgawanyiko wa majukumu.

Penye wengi pana mengi hivyo mgawanyo wa majukumu ni muhimu ili kazi ndani ya koloni iendelee kwa ufanisi. Koloni la Nyuki linaundwa na washirika wa aina tatu yaani Malkia, Wafanyakazi na Nyuki dume.

Malkia

Nyuki Malkia ana umbo kubwa kuliko Nyuki wengine wote huku mabawa yake yakiwa mafupi. ukubwa huu unatokana na huduma za pekee anazozipata kutoka kwa wafanyakazi.
Kazi yake pekee ya malkia ni kutaga mayai ambayo hupitia hatua zote za ukuaji hadi kufikia Nyuki wakubwa na kuingia kwenye majukumu ya kila siku.

Wafanyakazi
Majukumu ya Nyuki wafanyakazi ni kujenga, kulinda, kufanya usafi, kuhakikisha mzunguko wa hewa ndani ya Mzinga kwa kupigapiga mabawa yao na kutafuta chakula cha kutosha kwa ajili ya malkia na watoto.
Shughuli ya kutafuta chakula sio mchezo, wafanya kazi hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta maua mengi kwa ajili ya malighafi ya chakula chao. Tafiti zinaeleza kuwa kwa safari moja ya kwenda kutafuta chakula, Nyuki hutembelea takribani maua 100.

Ndani ya mzinga hubaki nyuki wengine ambao kazi yao ni kupokea malighafi hizo na kuzichakata ili kukamilisha asali. Nyuki wafanyakazi ni wadudu wakorofi na wakali; hukabiliana na yeyote anayehatarisha usalama wa malkia wao bila kujali kama wanahatarisha maisha yao.

Nyuki dume
Kwa upande mwingine Nyuki dume hawana kazi yao ni kuzaliana tu, inaelezwa kuwa wakati mwingine dume hutegemea wafanyakazi wampe chakula.

Nyuki wafanyakazi huishi kwa wiki sita tu.

Wakati binadamu wanatamani kuishi miaka 70,80, 90 au 100, Malkia Nyuki huishi kwa miaka 5 tu akiwa nyuki pekee anayeishi muda mrefu huku Nyuki wafanyakazi wakiishi kwa wiki tano hadi sita tu.

Malkia hutoa kemikali maalum zinazozuia Nyuki wengine kuzaliana.

Malkia Nyuki ndio Mama wa Nyuki wote kwenye koloni, hakuna Nyuki mwingine mwenye uwezo wakutoa mayai kwani hutoa kemikali ama pheromones zinazozuia majike wengine kuzaliana na hivyo kuwalazimu kuwa wafanyakazi wake Maisha yao yote.

Nyuki wafanyakazi huandaa malkia ajaye.

Uwepo wa malkia unadhihirishwa na uwepo wa pheromone anazozitoa. Pheromone za Malkia wa Nyuki zinapoisha huashiria kuwa malkia hawezi tena kutawala hivyo wafanyakazi huanza mchakato wa kumlea malkia wa dharura.
Wanaanza kujenga vyumba kwa ajili ya mabuu wachanga 10 hadi 20 wa kike ambapo mmoja wao atakuwa malkia anayefuata.

Wafanyakazi huwalisha malkia hawa watarajiwa chakula maalum almaarufu royal jelly chenye uwezo wa kuunda malkia mwenye ovari nzima zinazoweza kuzalisha mayai yenye rutuba.

Malkia wa kwanza kutoka kwenye buu, huwaua malkia wenzake waliolelewa Pamoja ili kuhakikisha yeye ndio wa kwanza n awa mwisho. Ikiwa wawili wataibuka kwa wakati mmoja, basi wawili hao watakuwa na vita vya kufa na kupona. Malkia atakayeshinda huanza harakati za kutaga mayai na kumiliki koloni.

Maisha ya wadudu hawa wadogo yamejaa mambo mengi yanayodhihirisha uthamani na upekee wake ulimwenguni .Hizi ni baadhi tu ya sifa na tabia za Nyuki bado kuna mengi ya kujifunza na kugundua.

Likes:
0 0
Views:
2968
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife