Waziri wa Maliasili na Utalii azuru eneo lenye nyayo za Binadamu wa kale

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kazi nzuri ya uhifadhi wa eneo la Laitole lililobeba historia muhimu ya Chimbuko la asili ya Mwanadamu.

Dkt. Chana licha ya kutoa pongezi hizo ameushauri uongozi wa Mamlaka hiyo uangalie namna bora ya kuliboresha eneo hilo lenye nyayo zinazosadikiwa kuwa ni za binadamu wa kale walioishi miaka milioni 3.6 iliyopita ili liweze kuiingizia Serikali mapato zaidi kutokana na Utalii.

Aidha, Dkt. Chana ameongeza kuwa kazi aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya Utalii kupitia Filamu ya Tanzania The Royal Tour inapaswa kuungwa mkono kwa Idara na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha, kuendeleza na kubuni vyanzo vipya vya mazao ya utalii ili kukidhi mahitaji na wingi wa watalii wanaoingia nchini.

Kwa upande wake Meneja wa Ulinzi wa Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi , Elibarick Bajuta amesema Mamlaka hiyo itayafanyia kazi maelekezo ya Waziri Balozi Dkt Chana ili eneo hilo liweze kukidhi kiu kubwa ya Watalii wanaotembelea Hifadhi hiyo.

Likes:
0 0
Views:
447
Article Categories:
Tourism