Siku ya UTALII Duniani

Takriban asilimia 40 ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya uhifadhi. Hii inajumuisha hifadhi za Taifa 22, eneo la hifadhi ya Ngorongoro, mapori tengefu, hifadhi za misitu asilia na misitu ya kupandwa, maeneo ya kihistoria pamoja na hifadhi za bahari. Maeneo yote hayo ndio kitovu kikubwa cha utalii nchini Tanzania.

Kutokana na mchango mkubwa wa utalii katika pato la taifa, ni muhimu kwa watanzania wote kuadhimisha tarehe 27 septemba ambayo ndio siku ya utalii duniani. Siku hii imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka kuanzia mwaka 1980.

Katika kutambua umuhimu wa utalii nchini, desemba 2018 chaneli ya Tanzania safari channel ilianzishwa mahsusi katika kutangaza vivutio vyote vya utalii nchini kwa malengo makubwa ya kukuza utalii na kuhamasisha uhifadhi nchini.

Tanzania safari channel inatumika kama nguzo muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu utalii wa ndani kwa maana vipindi na Makala zote zinahusu masuala na maeneo, mbalimbali ya utalii nchini Tanzania.

Hata hivyo, harakati za kukuza na kutangaza utalii nchini haukuishia hapo, Rais Samia Suluhu Hassan, alitia nia katika kuitangaza nchi kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour iliyofanikiwa kutangaza vivutio vingi vinavyopatikana nchini, ikiwemo historia ya Tanzania, utamaduni na maliasili zilizopo.

Siku hii ni muhimu sana katika kuhamasisha watu kutalii na kuhamasisha wale wanaofanya kazi katika sekta hii. Ikiwemo wahifadhi walio mstari wa mbele kuhakikisha rasilimali za utalii za taifa la Tanzania hazipotei ili tuweze kuwarithisha vizazi vijavyo.

Upekee wa vivutio vinavyopatikana nchini unaifanya Tanzania kujulikana kimataifa, mathalani tuzo za utalii duniani zinazo julikana kama world travel awards zimewahi kuitangaza Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi ya Taifa bora barani Afrika kwa mara tatu mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Serengeti ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania yenye eneo la kilometa za mraba 14,763, zilizosheheni madhari ya tambarare za nyasi. Hii ndio sehemu pekee duniani iliyobakia na maandamano ya kundi kubwa la Wanyama wanaohama ikiwemo nyumbu Zaidi ya milioni mbili, pundamilia na swala tomi. Kila mwaka, idadi kubwa ya watalii kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni hutia nanga katika ardhi ya Tanzania ili kujionea mamilioni ya Wanyama wanaohama yaani The Great Serengeti migration.

Mlima Kilimanjaro pia umeshinda katika tuzo hizi kwa mara nne mfululizo katika kipengele cha Kivutio bora cha utalii Afrika kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2018.

Kilimanjaro ndio mlima mrefu Zaidi barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari. Lakini pia ndio mlima mrefu Zaidi duniani usio katika safu za milima mingine. Mlima huu umekuwa chanzo cha kuvutia watalii wengi kutoka katika kila pande ya dunia, wengi wanakuja kustaajabu uzuri wa mlima huu.

Tanzania pia imetajwa kuwa nchi yenye uzuri asilia kuliko nchi zote barani Afrika katika taarifa iliyoandikwa na jarida la Forbes. Taarifa hii imetokana na mtandao wa money.uk ambapo nchi 50 ziliingia katika kinyanganyiro hiko na Tanzania ikashika nafasi ya nne duniani ikiwa ndio nchi ya afrika pekee kuingia katika nchi tano bora.

Katika taarifa hiyo maksi zilikusanywa kutokana na utafiti uliofanywa na tovuti ya money.uk na Tanzania ilipata alama 6.89 kati ya 10 na kuzipita nchi nyingine 46. Alama hizo zinatolewa baada ya kuhesabu vivutio asilia vya utalii vinavyopatikana katika maeneo husika ikiwemo milima na maeneo mengine ya uhifadhi.

Hakika Tanzania ni nchi iliyo na rasilimali nyingi za utalii zilizohifadhiwa kikamilifu ili kuvutia watalii duniani lakini pia kama nguzo ya kutunza mazingira na kuweka dunia kuwa sehemu salama kwa binadamu na viumbe wengine.

Kwakusema hayo, tunapozungumzia utalii duniani, basi nchi ya Tanzania itasimama katika kuelezea maana na faida za utalii kwa kutumia uwepo wa vivutio vingi vya asili na vya kipekee vinavyoakisi uzuri wa Tanzania unaovuta watu kutoka kona mbalimbali ulimwenguni.

Likes:
0 0
Views:
606
Article Categories:
Uncategorized