Mfahamu Konokono, kiumbe mwenye jinsia mbili, meno 1000

Mwili wa Konokono umeundwa na misuli laini inayotoa majimaji. Uwepo wa maji maji yanayotolewa na mwili wake unamsaidia Konokono kuwa salama dhidi ya miale mikali ya jua na bacteria huku utelezi wa maji hayo ukisababisha vitu  vyenye ncha kali kuteleza juu ya misuli yake na  hivyo kuepusha kumuumiza. 

Ganda la  konokono sio urembo tu

Mwili wa Konokono unabeba ganda gumu ambalo kwa wengi hulitambua kama urembo. Nyumba ya konokono imewekwa kwa ajili ya kazi maalumu huku ulinzi ukiwa dhumuni kuu. Ganda hulinda sehemu ndani kama vile moyo, mapafu na viungo vyake vya uzazi katika maisha yote ya Konokono. Vile vile Konokono hujikinga dhidi ya maadui kwa kujiviringisha na kujificha ndani ya gamba lake kila anapohisi hatari.

Konokono anahitaji unyevu muda wote

Mwili wa Konokono lazima ubaki na unyevu, vinginevyo Konokono hukauka na kufa. Hali ya hewa inapokuwa ya joto na kavu sana, Konokono hutambaa hadi mahali salama (kama juu ya kuta za nyumba) na kuvuta mwili wake ndani ya ganda kabla ya kuifunga ganda kwa kuziba maji maji yake. Hujifungia humo muda mrefu mpaka itakapomlazimu kutoka au joto litakapo shuka.

Ganda la Konokono linatambulisha umri wake

Ganda lake haliachi kukua, linaendelea kukua kadiri Konokono anavyozidi kukua, hii ndio kusema ukubwa  wa nyumba ndio ukubwa wa Konokono kiumri.

Konokono anaweza kutembea umbali wa Kilomita moja kwa takribani wiki moja.

Pia ni miongoni mwa viumbe vyenye mwendo mdogo sana, inaelezwa kuwa kama Konokono wangeweza kutembea bila kukatisha safari wangetumia wiki nzima kukamilisha umbali wa Kilomita 1.

Mwendo huu wa kusuasua unatokana na tabia yake ya kutembea kwa kuvuta misuli yake ambapo kabla ya kujivuta hulazimika kwanza kujikamua kutoa majimaji ya kumwezesha misuli yake kuteleza wakati wa kujivuta.

Shughuli ya kutoa majimaji inatumia nguvu nyingi, hivyo analazimika kwenda taratibu ilikukusanya nguvu. Tabia hii pia inatoa majibu ya alama ya majimaji inayoachwa na kila anapopita.

Konokono anaweza kula kila kitu inapomlazimu

Aina ya chakula cha Konokono inategemea na mahali anapopatikana. Konokono wa nchi kavu ni hebivora yaani wanakula majani, matunda na magome ingawa baadhi yao ni omnivora, yaani wanakula kila kitu huku wengine wakipendelea zaidi vitu vilivyokufa kama majani au magogo yaliyooza.

Konokono ana zaidi ya meno 1000

Licha ya tofauti za chakula, meno ya Konokono ni tofauti kabisa na wanyama wengine. Ana meno mengi yanayoweza kufikia au hata kuzidi 1200 na madogo sana ambayo ni ngumu kuyaona kwa macho ya kawaida. Meno hayo yamepangwa kwenye ulimi wake na humsaidia kukwangua  sehemu laini za chakula chake wakati wa  kula. Kutokana na shughuli hii ya kukwangua chakula meno ya Konokono hubadilishwa mara kwa mara. 

Konokono mmoja ana jinsia mbili (Hermaphrodites)

Konokono haishiwi maajabu. Wakati ni nadra sana kwa mnyama mmoja  kuwa na jinsia mbili, Konokono wengi wanajinsia mbili hivyo hawalazimiki sana kuingiliana japokuwa baadhi ya Konokono, hasa wanaopatikana kwenye maji, huweza kufanya hivyo kwa sababu jinsia zao zimetengana, yaani kuna konokono kike na dume.

Mzunguko wa maisha ya viumbe hawa wenye tabia za pekee mara nyingi huwa mwaka mmoja lakini wengine huweza hadi miaka 10  wakiwa nyikani.

Likes:
0 0
Views:
1657
Article Tags:
Article Categories:
History