Detepwani, ndege ambaye macho yake yameipinga fizikia

Detepwani ni miongoni mwa ndege wengi wanaotegemea na kupatikana pembezoni mwa Ziwa Victoria na vyanzo mbalimbali vya maji. 

Ndege huyu maarufu kama PIED KINGFISHER kwa lugha ya kigeni amejipatia umaarufu mkubwa katika maeneo mengi duniani kwa sababu ya tabia zake za pekee hasa wakati wa kutafuta chakula.

Detepwani anatokea kwenye familia kubwa ya ndege wenye ukubwa wa wastani, kichwa kikubwa, mdomo mrefu uliochongoka, miguu mifupi na mkia mfupi ambao kwa pamoja huitwa Chopoa au Mdiria kwa Kiswahili huku kitaalam familia hii ikijulikana kama Alsedinidae. 

Ndege hawa wa ajabu licha ya kutofautiana majina na mwonekano, baadhi ya tabia zao pia zinatofautiana, wakati Detepwani ni bingwa wa kuwinda na kuvua samaki kama chakula chake kikuu, Chopoa wengine hawali samaki kabisa badala yake wanawinda wadudu na mijusi kwa ajili ya chakula.

Pengine tofauti hii inatokana na utofauti wa mazingira ambayo ndege hawa wa familia moja wanapatikana. Chopoa wanaokula wadudu wanapatikana zaidi msituni ambapo kuna wadudu wengi wa kutosheleza mlo wao huku Detepwani akipendelea maeneo ya maji, kama vile karibu na mito, mabwawa na maziwa ambapo samaki na viumbe vya majini vipo kwa wingi.

Chopoa wengine wanaokula samaki ni pamoja na Kisharifu ama kwa kigeni Malakait Kingfisher na Mkumburu yaani Giant kingfisher.

Detepwani ana rangi za pekee tofauti kabisa na Chopoa wengine, mwili wake umefunikwa na manyoya ya madoa meusi na meupe huku mdomo wake uliochongoka kama kisu ukiwa mweusi.

Ingawa mara nyingi Detepwani huonekana angani akitafuta chakula, wakati mwingine anapumzika kwenye miti akipiga mahesabu na kusasisha mbinu zake za kujipatia chakula kwa wakati. Miguu yake midogo inamwezesha kufanya hivyo kwani ina vidole vinne ambavyo humuwezesha kujishikiza vizuri kwenye matawi ya mti bila kuteleza wala kuanguka.

Maandiko matakatifu yanaasa kuwa asiyefanya kazi na asile, vivyo hivyo kwa viumbe wa porini pia. Mchakato wa chakula kwa Detepwani ni kazi nzito inayohitaji mbinu na umahiri mkubwa, kwani upatikanaji wa chakula unategemea uwezo wake wa kuona samaki aliye majini na kumkamata kwa wakati.

Kwa kutambua kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, Detepwani amejijengea uhodari mkubwa wa kuwinda na kuvua samaki kuliko Ndege wengine wa jamii yake. Uhodari huu unatokana na uwezo wake wa kushuka kwenye maji kwa kasi kubwa na ya ajabu ili kukamata samaki hata kabla samaki mwenyewe hajashtuka kama yupo hatarini. 

Tafiti zinaeleza kuwa Detepwani anashikilia rekodi ya kuwa ndege mkubwa mwenye uwezo wa kukaa sehemu moja angani akiwa anapaa yaani Hovering.

Akiwa angani hana papara ya kuingia kwenye maji badala yake anatumia muda wa kutosha kuhakikisha kuwa anapata shabaha yake. Mahesabu anayopiga hapa ni umbali na mwendokasi wa kutumia ili kuhakikisha anainasa shabaha yake bila kukosa.

Ndege huyu ana uwezo wa kuruka juu mpaka usawa wa takriban mita 19 ambapo anaendelea kupiga mabawa yake kwa kasi kiasi cha kutengeneza taswira ya tarakimu namba 8, uwezo huu wa kupiga mabawa kwa kasi  unamwezesha asianguke chini huku mkia wake ukicheza kumpa balance ya kubaki sehemu moja asiende kulia wala kushoto. 

Detepwani hafanyi kazi bure, anavyoruka juu na kupiga mabawa yake akiwa sehemu moja ni mbinu inayompa nafasi ya kuelekeza macho yake chini kwa lengo la kuvuta taswira ya samaki aliyeko majini.

Kifizikia maji yana tabia ya kupindisha miale ya mwanga yaani kitu kilichopo nyuzi 90 ndani ya maji kinaweza kuonekana kama vile kipo nyuzi 45 kikitazamwa kutoka nje. Lakini fizikia hii imegonga mwamba kwa Detepwani kwani macho yake yameboreshwa kumuwezesha kuona kitu kikiwa sehemu ile ile bila taswira yake kupindishwa na hivyo kumwezesha detepwani kuona vizuri kabisa vitu vilivyopo ndani ya maji.

Baada ya kuhakikisha mahesabu yake, Detepwani hushuka kuelekea kwenye maji kwa kasi kubwa akitanguliza kichwa chini moja kwa moja kukamata shabaha yake. Kushuka kwenye maji na kuibuka tena ni kitendo cha haraka sana, ndani ya sekunde chache tu kila kitu kimekwesha na detepwani kuondoka.

Maisha ya Detepwani ni hadithi inayoburudisha, kufurahisha na kustaajabisha lakini pia yanatoa somo kuwa Subira, mikakati na kuchukua hatua kwa kujiamini ndio funguo ya mafanikio.

Likes:
0 0
Views:
783
Article Tags:
Article Categories:
Tourism