Maisha ya Ngiri na utofauti wake na Nguruwe wengine

Ngiri ni wanyama mashuhuri wanaotokea jamii moja na Nguruwe. Kichwa chao ni kikubwa na kipana upande wa nyuma, kikielekea kwenye pua ambayo ina pembe mbili za juu zilizopinda, kuanzia inchi 10-25 kwa wanaume na inchi 6-10 kwa wanawake. Taya zao za chini pia zina jozi ya pembe fupi ambazo zina ukubwa sawa kwa dume na jike.

Ngiri hawana mafuta ya ‘subcutaneous’ na wana koti ndogo sana inayowafanya kuathiriwa na joto kali la mazingira. Hivyo mara nyingi wakati wa joto wanyama hawa hujiviringisha kwenye tope ili kuifunika ngozi yao na kuikinga na miale mikali ya jua na joto.

Tofauti na nguruwe wengine, Ngiri hupendelea kula kwenye ncha za nyasi zinazochipua, mizizi, matunda, magome ya miti michanga na mara kwa mara mizoga.

Ngiri ni ‘polygynandrous’ yani jike huwa na wenza wengi na vivyo hivyo dume pia anaweza kuwa na majike wengi.

Ngiri ni mamalia hivyo wanauwezo wa kuzaa na kunyonyesha. Tofauti na Wanyama wengine jamii ya Nguruwe, Ngiri hubeba mimba kwa muda mrefu zaidi kuanzia siku 170 hadi 175.

Kabla ya kuzaliwa, majike hujitenga na kuzaa kwenye shimo, ambalo ni muhimu katika kudhibiti halijoto ya mwili kwani Ngiri wachanga hawawezi kudumisha joto lao la mwili katika siku chache za kwanza za maisha.

Baada ya kuzaliwa watoto wa Ngiri hukaa kwa wiki sita hadi saba kwenye shimo kabla ya kuondoka na mama yao. Madume hukaa kwenye kundi moja na mama hadi miaka miwili huku majike yakiendelea kuishi kundini hadi ukomavu wa kijinsia.

Hutumia muda mwingi wa siku kutafuta chakula na kwa kawaida hupatikana katika vikundi vidogo vya familia. Usiku, hutafuta makazi kwenye mashimo na kulala na kichwa chao kuelekea ufunguzi wa shimo; hii ni kuruhusu kutoroka haraka nje ya shimo pindi wanapohisi hatari.

Ngiri huishi katika mojawapo ya vitengo vitatu vya kijamii – kuna wale wanaopendelea maisha ya upweke hasa madume wakonge, vikundi vya madume wadogo mabachelor, na vikundi vya majike 4-16 na watoto wao wa jinsia mchanganyiko. Vikundi kadhaa vya Ngiri vinaweza kushiriki kwa amani rasilimali muhimu kama chakula ikiwa ziko nyingi lakini ushindani mkubwa hutokea pale ambapo rasilimali hizo hazitoshelezi.

Hutumia muda mwingi wa siku kuchunga au kugaagaa. Wakati wa kula wanyama hawa hukunja miguu yao ya mbele chini ili kufikisha vichwa vyao kwenye ncha za nyasi na kuegemea kwenye ‘vifundo’ vya mikono. Kinyume chake, wanapong’oa mimea wakati wa kiangazi, hutumia pua yao ngumu kusukuma udongo.

Ngiri wanapatikana maeneo mbalimbali nchini Tanzania na ni kivutio kikubwa cha utalii wa wanyamapori.

Likes:
0 0
Views:
1875
Article Categories:
Tourism