Mfahamu mnyama Nyamera

Nyamera ni mnyama anayefanana na kongoni na mwenye ukubwa wa kati na uzito unaoanzia kilogramu 75 mpaka 160. Mnyama huyu anapendelea zaidi kuishi katika maeneo ya uwanda wa nyasi wenye majira ya mafuriko. Kukosekana kwa mvua au mafuriko kwa kipindi kirefu kunaweza kupelekea idadi kubwa ya vifo vya Wanyama hawa.

Nyamera wanapendelea zaidi kula nyasi fupi au zile zinazoota baada ya eneo kuchomwa moto. Kama ilivyo kwa Wanyama aina ya Nyumbu, kuishi katika makundi makubwa husaidia Nyamera kuepuka maadui, lakini pia makundi hayo husaidia kuzikanyaga nyasi ndefu na baada ya muda nyasi mpya huota tena hivyo kuongeza nyasi fupi za chini zinazoweza kuliwa na Nyamera.

Makundi ya Nyamera yanaweza kuwa na mamia kwa maelfu ya Nyamera wanaozunguka kwa umbali wa takribani kilomita 1,000. Mzunguko huo unaweza kuwa pembezoni mwa mabonde au uwanda wenye nyasi rafiki. 

Majike wenye umri kati ya miezi 12 mpaka 28 huwa tayari kuzaa watoto wakati madume huwa tayari katika umri wa miezi 42. Katika kipindi cha kuzaliana, madume huingia katika mapambano ili kumpata jike aliye tayari kuzaa. Baada ya miezi 8 mtoto wa Nyamera huzaliwa, kisha kuchukua siku kadhaa kujiunga na mama yake. 

Kuanzia miaka 15 madume huanza kupoteza meno, na hii husababisha vifo kwa madume hayo. Majike wao huendelea kuzaa na kulea watoto hata baada ya kupoteza meno yote. 

Nyamera ni kati ya wanyama wenye mwendokasi wa juu kufikia kilomita 70 kwa saa ukilinganisha na wanyama wengine wa jamii yake. 

Nyamera wametoweka sana katika maeneo yao ya asili japo wanapatikana kwa wingi katika maeneo waliosalia. Unaweza kuwaona Wanyama hawa katika hifadhi na maeneo tengefu hapa nchini Tanzania.

Likes:
0 0
Views:
16
Article Tags:
Article Categories:
Tourism