Waigizaji wa India kutumia vivutio vya Tanzania kwenye filamu

Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan amesema Tanzania ipo katika nafasi nzuri kuvutia watalii wa ndani na wa nje ya nchi kutokana na kuwa na miundombinu mizuri huku mingine ikiwa katika maboresho makubwa.

Ameyasema hayo wakati wa mahoniano maalum na Tanzania News, chaneli ya Kiingereza ya mtandaoni iliyo chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Balozi Pradhan amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuweza kuunganisha karibia mikoa yote na barabara nzuri za lami, huku miundombinu ya reli ikiboreshwa kila siku na safari za majini zikiwa pia bora, hivyo miundombinu hiyo inavutia watalii kutembelea Tanzania na pia Watanzania wenyewe wanaweza kusafiri popote kwa njia rahisi.

Balozi Pradhan ameongeza kuwa atafanya jitihada za kuwakaribisha watengenezaji filamu wa India kuja kutumia mandhari nzuri za Tanzania hasa Zanzibar katika utengenezaji wao wa filamu.

Pia, ametoa pongezi serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwekeza nguvu kuvutia watalii kutia ndani kutengeneza kwa filamu ya Tanzania: The Royal Tour.

India ni moja ya nchi chache duniani zilizofanikiwa katika utalii wa ndani ambapo mamilioni ya Wahindi hutalii taifa lao na kuliingizia mapato. Pia watu wengi hutembelea taifa hilo kutokana na vivutio vyake, tamaduni na vyakula.

Likes:
0 0
Views:
750
Article Tags:
Article Categories:
Tourism