Mradi wa REGROW wanufaisha wakazi wa Madibira – Mbeya

Serikali kupitia mradi wa kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) unajenga Mfereji wa umwagiliaji wa Madibira uliofikia 49% kwa gharama ya zaidi ya bilioni 8.7 wenye lengo la kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati kwa ajili ya kilimo na pia maji katika Mto Ruaha mkuu yanaendelea kupatikana ili kusaidia katika matumizi ya wanyama na ekolojia ya Ruaha, na mwisho maji yanayobakia yanaenda kwenye mradi mkubwa wa kimkakati wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere.

Mfereji huo unahudumia kata mbili za Miyombweni na Madibira na vijiji 11 ambapo watu wake wanajishughulisha zaidi na kilimo cha Mpunga, ambapo zaidi ya wakulima elfu 3 wanategemea maji kwa ajili ya kilimo chao.

Wakizungumza na TBC, wakazi hao wameishukuru serikali kwa mradi huo, kwani takribani hekta elfu 3 za mashamba yao yanategemea maji, na kwa sasa wamekiri kupata maji kwa wakati, hivyo kuzalisha mavuno mengi kutokana na urahisi wa upatikanaji wa maji, kwani mifereji hiyo inapita katikati ya mashamba yao.

Na Wakandarasi wanaojenga mfereji huo ni kampuni za Kitanzania, ambapo kampuni ya SKYLINE imeungana na kampuni ya JV WHITE CITY, na wameipongeza serikali kwa fursa inayoendelea kuwapa wakandarasi wazawa, kwasababu mzunguko wa pesa unabaki nchini, na wameahidi kumaliza kazi ndani ya muda uliopangwa, ambao ni Januari mwakani.

Kwa upande wake Kaimu Msimamizi wa mradi wa REGROW Blanka Tengia amesema kuwa wamedhamiria kukuza utalii kusini, ambapo ili kufanikisha azma hiyo ni muhimu kuhakikisha rasilimali ambazo zipo ndani ya hifadhi kama vile wanyama na mimea vinatunzwa, pia ndiyo maana mradi huo umeleta tija kubwa katika kulinda maliasili, hivyo kuongeza utalii nchini.

Likes:
0 0
Views:
341
Article Categories:
TSC