Bilioni 14 kutatua migogoro ya binadamu na wanyamapori

Tanzania imepokea Euro milioni 10 (TZS bilioni 23.8) kutoka Ujerumani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na mradi wa kupunguza migogoro baina ya binadamu na Wanyamapori ambao una thamani ya Euro milioni 6 (TZS bilioni 14).

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati wa hafla fupi ya Kusaini Makubaliano Baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya Utekelezaji wa Miradi hiyo katika ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu leo jijini Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa katika wilaya za Serengeti, Bunda Vijijini, Tunduru, Mwanga, Mvomero, Namtumbo na Itilima kumekuwa na matukio mengi ya wanyamapori kusababisha madhara kwa wananchi na mazao ukilinganishwa na wilaya nyingine.

Katika kipindi cha miaka mitano (2017 – 2021), wastani wa wananchi 28,137 wamepata madhara kutokana na wanyamapori ikijumuisha uharibifu wa mazao (ekari 56,972) yenye thamani ya wastani wa shilingi bilioni 28, jumla ya wananchi 508 kujeruhiwa na 634 kuuawa na wanyamapori.

Likes:
0 0
Views:
481
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife