Maajabu ya nyoka na sifa zao

Nyoka ni viumbe wenye damu baridi, magamba yanayomeremeta jamii ya  mijusi wasio na miguu. Viumbe hawa wa ajabu wamebeba sifa nyingi zinazochochea upekee wao.

• Baadhi ya Nyoka wana uwezo wa kuzaa

Ingawa asilimia kubwa ya Nyoka kama vile Chatu na Koboko hutaga mayai (Oviparous), baadhi ya spishi za Nyoka  hurutubisha na kutotolesha mayai yakiwa ndani ya mwili (Ovoviviparous) huku wengine wakilea watoto wao kwenye placenta na kuzaa watoto hai kabisa (Viviparous). Mfano wa nyoka wanaozaa watoto ni pamoja na Nyoka maji, Anaconda, Nyoka njuga (Rattle snake).

• Asilimia 98 ya aina za Nyoka hawana Sumu

Kuna aina 3,000 za Nyoka duniani lakini aina 200 sawa na asilimia 2 tu ya Nyoka ndio wenye sumu. Nyoka wenye sumu hutumia sumu kwa lengo la kuwinda, kusaidia mmeng’enyo wa chakula na kujilinda dhidi ya adui lakini Nyoka wasio na sumu hutumia njia mbadala kuhakikisha wanapata chakula na kujilinda. 

Jamii zote za Chatu ni miongoni mwa Nyoka wasio na sumu hujipatia chakula kwa kulinyonga windo lake na kulivunjavunja kabla ya kulimeza, kadiri mhanga (windo) linavyovuta pumzi ndivyo chatu huongeza bidii ya kunyonga. 

Mbali na kutafuta chakula, Nyoka wasio na sumu hujikinga na maadui kwa  kuwang’ata ili kusababisha maumivu, kujifananisha na mazingira, kujiviringisha ili kuficha kichwa, kutetemesha mkia na wengine hujisugua magamba ili kutoa sauti ya kumtisha adui lakini hatari inavyokuwa kubwa sana Nyoka hukimbia kwa usalama wao. 

• Nyoka hutumia magamba yao ya chini kama miguu

Wakati  viumbe wengine wakitumia miguu na mabawa kutembea na kukimbia na kuruka, Nyoka wanatumia magamba yao ya chini kama miguu. Magamba haya yameungana na misuli yake hivyo yanapojivuta na kuachia humwezesha kusonga mbele.

• Nyoka hawana kope wala masikio

Tofauti  na reptilia wengine Nyoka ni mnyama asie na kope machoni wala masikio ya nje hivyo  hutegemea vishindo vya ardhi na kutumia  ngozi  na ulimi wake ili kujua uelekeo na kusikia vishindo vya vitu au viumbe wengine.

• Nyoka hujifananisha na mazingira

Nyoka wanapatikana maeneo mbalimbali kama vile kwenye maji, juu ya miti, kwenye vichaka, shimoni na kwenye mapango. 

Kukosa miguu na uwepo wa maadui wengi huwalazimu Nyoka kuwa na rangi zinayoshabihiana na mazingira kwa lengo la kujificha kutoka kwa maadui zao hususani ndege ambao huwavizia kutoka angani. Pamoja na hilo kushabihiana na mazingira  pia ni mbinu ya kufanikisha mawindo kwani kunafanya windo lake lishindwe kumtambua na  hivyo kurahisha upatikanaji wa chakula.

• Ngozi ya Nyoka haiwezi kutanuka

Tofauti na wanyama wengine ambao ngozi zao huwaruhusu kurefuka, kunenepa na kuongezeka, uwepo wa magamba kwenye ngozi ya Nyoka huzuia ukuaji wake hivyo  Nyoka analazimika kujivua magamba kila baada ya muda fulani kulingana na umri na jamii ya Nyoka husika. 

Kwa wastani Nyoka mkubwa anaweza kujivua gamba mara tatu hadi nne kwa mwaka lakini Nyoka mdogo hujivua gamba hata kila baada ya wiki mbili. 

Tabia ya kujivua gamba ni muhimu sana kwa maisha ya Nyoka kwani inamwezesha katika ukuaji yaani pasipo kuvua magamba  basi mwili wa Nyoka hauwezi kukua.

Hizi ni baadhi tu sifa nyingi za viumbe hawa wa ajabu. Kumbuka hakuna sifa ya ujumla kimaumbile au mwonekano inayoweza kusaidia kutofautisha Nyoka wenye sumu na wasio na sumu ndio maana ni muhimu kukaa na nyoka kwa tahadhari kubwa. 

Likes:
0 0
Views:
76
Article Tags:
Article Categories:
HistoryTourismWildlife