Utofauti wa Palm-nut vulture na ndege wengine

Ni ndege wanaopatikana maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo yalipo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika.

Ndege huyo ana tabia za pekee tofauti kabisa na ndege wenzao jamii ya Tumbusi.

Wakati Tumbusi wengine wakitegemea nyama pekee kwa ajili ya chakula, Palm-nut vulture hutegemea zaidi mitende kama chakula chake kikuu, ingawa mara moja moja hutumia wadudu na samaki kupata virutubisho zaidi au kukidhi mahitaji ya njaa wakata wa uhaba wa chakula.

Tabia za Palm-nut vulture mara zote zimekuwa za kipekee. Ndege hawa watulivu hupendelea kuishi maisha ya upweke. Hawapendi makundi na Dume huwa na mwenza (Jike) mmoja tu.

Unapofikia msimu wa kuzaliana wenza hao hushirikiana kuandaa kiota juu ya matawi ya mti huku wakisubiri kifaranga wao.

Kiota chao hutengenezwa kwa malighafi mbalimbali ikiwemo vijiti vigumu, nyasi na kinyesi ili kukipa ustahimilivu kinapokuwa tawini.

Cha kushangaza ni kuwa jitihada zote zinazofanywa na wenza hao, huambulia kifaranga kimoja tu. Hii ndio kusema kila msimu wa kuzaliana ambao ni Agosti na  Septemba, Palm-nut vulture hutaga yai moja pekee.

Ushirikiano wa ndege hawa huendelea kutoka kujenga kiota kulea mayai kwa siku 42 (wiki 6) hadi kulea na kulinda kifaranga kitakachototolewa. Katika harakati zote hizi Dume wa Palm-nut vulture hamuachi mwenzake, huendelea kuwa pamoja.

Likes:
0 0
Views:
554
Article Tags:
Article Categories:
TourismWildlife