Zifahamu zifa za buibui na nguvu ya utando wake

Zaidi ya aina 45,000 za buibui zinajulikana duniani kote. Tafiti zinaonesha kwamba aina nyingi za buibui hawana madhara kwa binadamu bali kwa wadudu wengine.

Buibui wengi ni kanivora, yaani wanakula na kuwinda wadudu kwa kutumia utando au uwindaji wa kawaida.

Utando huu pia unaweza kutumika kutambua na kutofautisha aina mbalimbali za buibui.

Sifa kubwa ya mdudu buibui ni uwezo wake wa kutengeneza hariri au kwa kiingereza huitwa Silk. Hariri ni nyuzi nyuzi imara za protein zinazotengenezwa ndani ya mwili wa buibui ambazo zinazomsaidia buibui kujenga utando, kupanda kwenye miti au majengo, kutengeneza viota na kazi nyingine nyingi ikiwemo kupunguza wadudu waharibifu kwenye mimea na mazao ya shambani.

Japo buibui wote hutengeneza hariri si buibui wote hujenga utando. Utando ni sifa kubwa ya buibui. Umahiri wa buibui katika kutengeneza utando kwa maumbo mbalimbali unaweza kukuacha mdomo wazi.

Utengenezaji wa utando ni upekee aliojaaliwa buibui, yaani anazaliwa akiwa tayari na uwezo, ustadi na ujuzi wa kutengeneza.

Nyuzi za hariri zinaweza kuwa nene au nyembamba, kavu au zenye maji maji, buibui mwenyewe huamua anahitaji hariri ya aina gani na kwa kazi ipi. Mara nyingi unaanza na nyuzi zenye maji maji ambazo huendelea kukauka zinapokuwa hewani.

Wakati wa kuanza shughuli ya ujenzi wa utando, buibui atatoa nyuzi za hariri ambazo zitajishikiza sehemu husika, kwenye tawi la mti au kona ya chumba au sehemu yoyote alipodhamiria kujenga utando huo.

Huku akiendelea kutoa nyuzi za hariri, buibui ataendelea kwenda mbele na kurudi nyuma kuufanya utando kuwa bora na imara Zaidi na wenye mpangilio maalum.
Shughuli yote hii haifanywi bure. Utando huu ni nyenzo muhimu katika shughuli ya uwindaji. Endapo wadudu, hasa wadudu wapaao ataruka karibia na utando basi atanaswa kwenye utando huo na kuishia kuwa kitoweo cha buibui.

Lakini unaweza kujiuliza Je! kwanini buibui mwenyewe hawezi kunasa kwenye utando wake?
Jibu ni kwamba, buibui anamkusanyiko wa mafuta mafuta kwenye miguu yake ambao ndio unamsaidia asiweze kunasa kwenye utando huo.

Si buibui wote hutegemea utando katika kujipatia kitoweo cha kila siku, Buibui wengine huwinda kwa kuwakimbiza wadudu ardhini.

Buibui wengi wana macho manane, wachache huwa na macho sita. Pamoja na kuwa na macho yote hayo, buibui wengi wana uoni hafifu.

Likes:
0 0
Views:
1558
Article Categories:
Wildlife